Papa atuma salam na matashi mema kwa wananchi wa Lebanon na Yordan
Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki
anafanya hija ya kichungaji nchini Lebanon na Yordan. Pamoja na mambo mengine Kardinali
Sandri anashiriki katika Ibada na maadhimisho mbali mbali ya Kiliturujia pamoja na
Maaskofu na Waamini wa Makanisa ya Mashariki. Ziara hii ambayo ameianza hapo tarehe
24 Mei, 2013 inatarajiwa kukamilika hapo tarehe 30 Mei 2013.
Lengo kuu la hija
hii ya kichungaji ni kwa ajili ya kuombea amani nchini Syria, Lebanon na Mashariki
ya Kati kwa ujumla. Kardinali Sandri anapenda kuwajulisha viongozi wa dini, waamini
na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, hija hii ya kichungaji inalenga zaidi kuonesha
moyo wa mshikamano na upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, anawaombea
na kuwapatia baraka zake za kitume katika: matumaini, shida na mahangaiko yao ya kila
siku.
Katika hija yake, Kardinali Sandri atapata pia fursa ya kuzungumza na
viongozi wa Makanisa ya Mashariki, Jumuiya za Kitawa, lakini kwa namna ya pekee na
vijana wanaoendelea kujitolea kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi kutoka Syria. Hawa
ni wale vijana ambao wanashirikiana bega kwa bega na Caritas Lebanon.
Baba
Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu tatizo la wakimbizi anasema kwamba, Jumuiya
ya Kimataifa haiwezi kuendelea kukaa kimya wakati watu wanateseka kiasi hiki kwa kupokonywa
haki zao msingi. Wakimbizi wanalazimika kuyahama makazi yao kwa nguvu, changamoto
kwa Jumuiya ya Kimataifa na Kanisa kuwasaidia kwa hali na mali.
Kardinali
Sandri akiwa nchini Jordan atazungumza na viongozi pamoja na waamini waliko kwenye
eneo hili. Alhamisi tarehe 30 Mei, Kardinali anatarajiwa kuhudhuria uzinduzi wa Chuo
Kikuu cha Kikatoliki cha Madaba, kinachomilikiwa na kuendeshwa na Upatriaki wa Yerusalemu.
Tukio hili la kihistoria linatarajiwa kuhudhuriwa na Mfalme Abdallah wa pili kutoka
Yordan.
Kabla ya kurejea mjini Roma, Kardinali Sandri atatembelea kambi ya
wakimbizi waliokimbia kutoka Syria na baadhi ya nchi zilizoko Mashariki ya Kati, ili
kujionea mwenyewe hali halisi pamoja na kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa
Baba Mtakatifu Francisko anayeendelea kufuatilia kwa karibu zaidi hali ya wakimbizi
huko Mashariki ya Kati.