Wakimbizi kuwezeshwa katika sekta ya elimu ili kukabiliana na changamoto za maisha!
Shirika la kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Shirika la
Wayesuit la Kuhudumia Wakimbizi, hivi karibuni wametiliana sahihi mkataba wa ushirikiano
unaopania kuwajengea uwezo wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi kwa kuwapatia elimu
ya juu kwa njia ya mtandao katika nchi zile ambazo UNHCR na JRS zinatekeleza majukumu
yake.
Wakimbizi
na watu wasiokuwa na makazi wanakabiliana na hali ngumu ya maisha, kiasi kwamba, mara
nyingi wanajikuta wako pembezoni mwa Jamii. Elimu ni njia makini inayoweza kuwajengea
uwezo wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi, ili kuweza kuwajibika barabara katika
maboresho ya maisha na Jamii inayowazunguka. Elimu ni njia nyingine inayoweza kutumika
pia kuponya madonda ya utengano, chuki na uhsama ndani ya Jamii, kwa kukazia mambo
yanayowaunganisha zaidi.
Kuna wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi nchini
Yordan, Kenya na Malawi ambao tayari wamekwishajiandikisha kushiriki katika mpango
huu wa elimu ya juu kwa njia ya mtandao. Wanafunzi hawa wanasoma kwenye Vyuo Vikuu
vya: Regis kilichoko Marekani pamoja na mtandao wa Vyuo vikuu vya Wayesuit vilivyoko
nchini Marekani.
Mpango huu unatarajiwa pia kupanuliwa na hivyo kuzishirikisha
nchi nyingine kutoka Barani Afrika. Mipango inaendelea huko nchini Chad ili kuwawezesha
wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi kutumia fursa ya elimu ya juu kwa njia ya mtandao
ili kujiendeleza zaidi.
Elimu ni sehemu ya haki msingi za binadamu na ni kati
ya vipaumbele vinavyotolewa na Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa
katika mikakati yake ya maendeleo. Masomo ya elimu ya juu kwa njia ya mtandao yanatarajiwa
kwa siku za usoni kuendelea kuhusisha lugha kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Inapania
pamoja na mambo mengine kuwajengea uwezo wakimbizi na jumuiya zinazowahifadhi.
Kwa
upande wake, Shirika la Wayesuit kwa ajili ya kuwahudumia Wakimbizi linasema, kwa
wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum wanaosoma kwenye vyuo vyao vikuu watahudumiwa
kwenye eneo hilo na kusaidiwa na Majaalim kutoka katika vitivo wanavyohudumia. Hadi
sasa kuna idadi ndogo sana ya wakimbizi na wahamiaji waliobahatika kupata elimu ya
juu kwa njia ya mtandao.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari yanaiwezesha
Jumuiya ya Kimataifa kuwafikishia hata wakimbizi elimu ya juu mahali walipo. Ni matumaini
ya viongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi kwamba, makubaliano
haya yataendelea kuboreshwa zaidi na kuwa ni sehemu ya hali halisi na wala si jambo
la kushangaza.
Kunako Mwaka 2012 Shirika la kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa lilizindua mpango mkakati wa miaka mitano unaopania kuongeza kiwango cha idadi
ya wakimbizi wanaoshiriki kupata elimu ya juu. Mkataba huu pia unaendelea kuimaarisha
ushirikiano kati ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na Mashirika ya kidini katika
kuwahudumia wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum.
Bwana Antònio Guterres,
Kamishina mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi anasema Mashirika ya kidini yana
mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene,
hali ambayo inasaidia pia kuwalinda wakimbzi na wahamiaji.