vita na machafuko DRC ni tishio la amani, ustawi na maendeleo ya Nchi za Maziwa Makuu!
Machafuko ya kisiasa, kinzani na vita inayoendelea kufuka moshi nchini DRC ni kati
ya mambo ambayo yanahatarisha amani, ustawi na maendeleo katika nchi za Maziwa Makuu.
Ni maneno ya Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati wa ziara yake
ya kikazi nchini Msumbiji, DRC na Rwanda, wakati huu, Umoja wa Afrika unapoadhimisha
Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika.
Vita
inayoendelea nchini DRC imekuwa ni sababu ya kuibuka kwa makundi makubwa ya wakimbizi
wanaoyahama makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao. Katika ziara hii,
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amekagua miradi inayogharimiwa na Umoja wa Mataifa
mintarafu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015.
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa anabainisha kwamba, licha ya ukata uliosababishwa na myumbo
wa uchumi kimataifa, lakini bado Umoja wa Mataifa unapania kuhakikisha kwamba, Malengo
ya Maendeleo ya Millenia yanafikiwa. Hii ni pamoja na kutenga asilimia 0.7 ya pato
ghafi la taifa kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maendeleo.