2013-05-23 08:26:17

Haki, toba na msamaha ni mambo muhimu katika kudimisha amani na utulivu ndani ya Jamii!


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria limeonya kwamba, wananchi wa Nigeria wameteseka sana kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyoendeshwa na Kikundi cha Boko Haram. Serikali inaweza kutoa msamaha, lakini ikumbukwe kwamba, msamaha unakwenda sanjari na haki, vinginevyo ni kufumbia macho maovu ndani ya jamii.

Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anabainisha kwamba, ili msamaha wa kweli uweze kutolewa, wahusika hawana budi kukiri makosa waliyowatendea wananchi wa Nigeria. Ni mwaliko pia wa kuendeleza majadiliano ya kina na wahusika wa pande mbali mbali, ili haki, amani na utulivu nchini humo viweze kurejea tena. Kikundi cha Boko Haram kimejiimarisha sana kana kwamba, ni Jeshi rasmi linaloendesha shughuli zake Kaskazini mwa Nigeria. Hivi sasa vimekuwa ni vikundi ambavyo vinajihusisha na utekaji nyara, ujambazi na mashambulizi ya kushtukizia kiasi kwamba, wananchi wanajikuta hawana uhakika wa usalama wa maisha na mali yao.

Maaskofu Katoliki Nigeria wanasikitika kusema kwamba, Kikundi cha Boko Haram kinaonekana kuishinda nguvu Serikali ya Nigeria. Maaskofu wanawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuiombea nchi yao kwani amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha pia mwanadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.