2013-05-22 15:15:19

Ukuu wa madaraka hata ndani ya kanisa ni kuhudumia wengine.


Hata ndani ya kanisa, ukuu wa maradaka umo katika kuhudumia wengine, ni ujumbe wa Papa kwa wote wanaotafuta kupanda ngazi katika madaraka na vyeo.
Papa anasema, hata ndani ya Kanisa, njia pekee ya kusonga mbele ni kutumikia na si kutumikiwa kwa kuwa, kwa Mkristo, maendeleo katika mamlaka maana yake ni kuwa myenyekevu zaidi katika kuhudumia , kama Yesu alivyokuwa. Papa pia alisisitiza kuwa, nguvu ya kweli ni huduma na si bidii za kutafuta vyeo katika mamlaka .
Papa Fransisko alieleza katika mahubiri yake ya wakati wa Ibada ya Misa, asubuhi Jumanne , katika Kanisa ndogo la Mtakatifu Marta ndani ya Vatican. Kati ya walioshiriki katika Ibada hii ni pamoja na Mkurugenzi wa mipango wa Radio Vatican, Padre Andrzej Koprowski aliyeandamana na wafanyakazi wa Redio Vatican na ofisi za utawala za Vatican na mahujaji na watalii kadhaa. Pia walikuwepo Maria Voce na Giarncarlo Falletti ambao ni Rais na Makamuw a Rais wa Kikundi cha Fokolare.
Katika homilia yake, Papa alisema, kwa Mkristu maendeleo ya kweli hupatikana katika unyenyekevu binafsi, kama Yesu alivyokuwa. uwezo na nguvu ya kweli katika utendaji ni katika huduma na kwamba hakuna nafasi ya nguvu ya mapambano ndani ya Kanisa.

Papa aliendelea kuyatafakari masomo ya siku akisema, katika somo la Injili ,Yesu anazungumza juu ya mateso yake mwenyewe. Hata hivyo wanafunzi wake, hawakuelewa na walianza kubishana kuhusu nani aliye mkuu kati yao.
Papa akizungumza juu ya sehemu hii yenye machungu, alibainisha kuwa utafutaji wa kuwa mkuu katika madaraka hata ndani ya kanisa, si jambo jipya, kwa kuwa lilikuwepo hata tangu wakati wa Yesu, kama ilivyosikika katika somo la Injili. Na Yesu anatoa jibu katika mabishano hayo akisema, anayetaka kuwa mkubwa kuliko wote na awe mtumishi wa wote. Kwa jibu hili, Yesu anatupa fundisho kwamba,uwezo na nguvu ya madaraka ndani ya kanisa ni huduma.
Uwezo wa mamlaka katika utumishi, unajionyesha katika uhalisi wake kwamba ni huduma, kama yeye mwenyewwe alivyosema, sikuja kutumikiwa ila kutumikia na huduma yake ilikuwa huduma ya Msalaba , ambako alijinyenyekeza hata mauti, naa, mauti ya msalaba kwa ajili yetu, ili kutukomboa sisi. Na hivyo kwa sisi wafuasi wake , hakuna njia nyingine katika Kanisa ya kusonga mbele ila kupitia huduma. . Kwa Mkristo maendeleo yake hupatikana katika unyenyekevu wa huduma yake. Kama hatuwezi kujifunza sheria hii ya Kristo, sisi kamwe, hatuwezi kuuelewa ukweli wa ujumbe wa uwezo wa Yesu.

Papa alisema kuwa maendeleo "ina maana ya kuwa myenyekevu, kwa maana ya daima kuwa tayari kuhudumia wengine. Katika Kanisa, aliongeza, mkubwa ni yule anayekuwa mtumishi wa wengi, ni mtu aliye tayari kuhudumia wengine. Hii ni sheria. Hata hivyo, alibainisha Papa Fransisko kwamba, tangu mwanzo wa kanisa mpaka sasa kumekuwa na mapambano ya kutafuta ukubwa ndani ya kanisa na katika huduma za kijamii , wengi wakidhani kuw amkubwa ni kutumikiwa, kama inavyojionyesha katika namna za mazungumzo kwa wanao utafuta ukubwa.

Papa alizigeukia pia hali za kawaida za kijamii akisema, mtu anapopewa cheo kikubwa kinachotupiwa macho na wengi , wengi humwonea kijicho wakisema ah, mwanamke huyu au baba huyu ameula kwa kuwa sasa ni rais wa chama. Neno hili kupandishwa cheo ni nzuri na tunalitumia pia katika kanisa. Lakini maana halisi ya kupanda cheo ni kubebeshwa msalaba. Anayekubali kupandishwa cheo, anapaswa kujua kwamba , sasa anatakiwa kuwa mnyenyekevu zaidi kuliko alivyokuwa hata awali. Ni kukubali kuwa mnyenyekevu zaidi kwa ajili ya kuhudumia wengi zaidi. Huo ndio ukweli wa maana ya kupanda cheo .
Papa kisha alikumbuka kwamba Mtakatifu Inyasi wa Loyola ambaye, katika mazoezi yake ya kiroho, aliomba kwa Bwana Msulubiwa, neema ya unyeunyekevu. Na hii, alisisitiza ndiyo nguvu ya kweli ya huduma ya Kanisa. Hii ndiyo njia ya kweli ya Yesu,. Kama Yeye ulivyo hudumia, pia ni lazima kwa Mkristu kumfuata katika njia hii ya huduma. Hiyo ndiyo nguvu ya uweza wote wa huduma kwa Kanisa.

Papa alieleza na kutolea sala ili kwamba, Bwana Mfufuka awajalie wafuasi wake wote neema kuelewa kwamba: uweza na nguvu halisi katika kanisa ni huduma. Na pia kuelewa kwamba, Sheria kuu aliyotufundisha katika mfano wa maisha yake kwa ajili ya maendeleo ya Mkristo, ni unyenyekevu.










All the contents on this site are copyrighted ©.