Jengeni utamaduni wa majadiliano ya kidini ili kukuza na kuimarisha misingi ya haki,
amani, upendo na mshikamano wa kweli!
Majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu sana katika kukuza na kudumisha utamaduni wa
haki, amani na utulivu. Hii ni changamoto kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia
ya tatu ya Ukristo Kanisa linapoendelea kujielekeza zaidi na zaidi katika mchakato
wa Uinjilishaji Mpya sanjari na kudumisha amani na utulivu, mambo msingi katika maendeleo
ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao
ya wengi ni kati ya mambo ambayo kimsingi yanapaswa kuongoza na kutoa dira na mwelekeo
wa majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Majadiliano
haya yajenge na kuimarisha ushuhuda wa waamini kwa Kristo na Kanisa lake; kwa pamoja
wasimamde kidete kupinga utamaduni wa kifo, wakijitahidi kuvumiliana na kuthaminiana,
kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Ni changamoto iliyotolewa
hivi karibuni na Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania wakati
wa mahubiri yake kwa Waamini wa Kanisa Katoliki kutoka katika Majimbo kumi na nne
ya Tanzania, wakati wa hija, kama sehemu ya Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria
wa Fatima sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Kwa kipindi cha siku tatu, mahujaji
hao wamesali na kulitafakari Neno la Mungu ambalo kimsingi linapaswa kuwa ni taa na
dira inayoongoza maisha yao ya kila siku.
Askofu Chengula anawaalika Wakristo
kujenga na kudumisha fadhila ya huruma, upendo na unyenyekevu; daima wakipania kushirikiana
na waamini wa dini na madhehebu mengine bila kuwasahau watu wenye mapenzi mema kwa
ajili ya maendeleo na ustawi wa wananchi wa Tanzania katika ujumla wao. Migogoro na
kinzani za kidini au kisiasa ni vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya mwanadamu.
Askofu
Chengula afafanua kwamba, kukosa na kukosehana ni sehemu ya ubinadamu, lakini kusamehe
na kusahau ni mwanzo wa njia ya utakatifu wa maisha. Msamaha na haki ni fadhila muhimu
sana katika ujenzi wa mshikamano wa upendo miongoni mwa Jamii. Waamini wajitahidi
kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vyao, pamoja na kumheshimu
binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Familia Takatifu ya Yesu,
Maria na Yosefu ni kielelezo makini cha fadhila za Kikristo, lakini zaidi katika:
kuhudumiana, kusaidiana na kuendeleza zawadi ya maisha kwa njia ya kufanya kazi kwa
juhudi, bidii na maarifa. Familia Takatifu iwe ni kioo cha tunu bora za maisha ya
kifamilia miongoni mwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Familia zijifunze
kusali, kutafakari Neno la Mungu pamoja na kulimwilisha kwa njia ya matendo ya huruma,
kama kielelezo cha imani tendaji, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka
wa Imani.
Wanafamilia wajitahidi kutoa malezi bora kwa watoto wao na wao wenyewe
wakionesha kuwa ni mfano wa kuigwa na Jamii inayowazunguka. Wawe imara kutekeleza
wajibu na dhamana yao ndani ya Familia na Jamii katika ujumla wake, kwani kimsingi
Familia inapaswa kuwa ni chimbuko la imani, matumaini na mapendo ya Kikristo.
Kila
mwamini kutokana na dhamana aliyojitwalia wakati wa Ubatizo na kuimarishwa kwa Sakramenti
ya Kipaimara anashiriki ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo katika hija ya maisha
yake hapa duniani. Waamini wajitahidi kulijenga na kulitegemeza Kanisa la Kristo kwa
hali na mali.
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga hija ya mahujaji
kutoka mikoa kadhaa ya Tanzania imehudhuriwa pia na Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo
Katoliki la Morogoro.