Hali ya hatari inapaswa kwenda sanjari na ushiriki wa wanasiasa katika kulinda na
kudumisha: haki, amani na utulivu nchini Nigeria
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria baada ya tafakari na upembuzi yakinifu linasema
kwa sasa linaunga mkono jitihada za Serikali ya Nigeria ya kupambana na Kikundi cha
Boko Haram Kaskazini mwa Nigeria kwa Serikali kutangaza hali ya hatari, kama sehemu
ya mkakati wa kudhibiti kikundi hiki ambacho kimekuwa ni chanzo kikuu cha maafa na
madhulumu ya kidini nchini Nigeria.
Hayo yamebainishwa na Askofu mkuu Ignatius
Ayau Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria wakati akizungumza na waandishi
wa habari hapo tarehe 21 Mei 2013. Ni matumaini ya Maaskofu kwamba, hatua zilizochukuliwa
na Serikali ya Nigeria ni kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Nigeria katika ujumla
wao. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, taifa linatumia rasilimali na fursa
zilizopo ili kutatua mgogoro huu ambao umekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya
wananchi wa Nigeria.
Wakati Serikali inaendelea kuimarisha juhudi zake kwa
njia ya vikosi vya ulinzi na usalama, lakini wanasiasa pia hawana budi kushiriki kikamilifu
katika mchakato huu unaopania kulinda na kudumisha haki, amani na utulivu nchini Nigeria.
Uchaguzi mkuu nchini humo kisiwe ni kisingizio cha kushindwa kudhibiti vitendo hivi
kwa kuogopa kunywima kura na watu wanaounga mkono kikundi cha Boko Haram.