Benki ya Vatican kuendelea kuimarisha misingi ya ukweli na uwazi katika utekelezaji
wa majukumu yake!
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amewaambia Mabalozi waliowasilisha hati zao
za utambulisho kwamba, fedha inapaswa kutumika katika mchakato wa kuwaletea watu maendeleo
na kamwe isiwe ni chambo cha kutaka kuwatala wa kuwagandamiza watu. Ukweli, uwazi
na maadili ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kupewa msukumo wa pekee katika masuala
ya fedha na uwekezaji. Hii ndiyo changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto wa kumi na sita, inayoendelea kuvaliwa njuga na Papa Francisko kwa sasa.
Kwa kuzingatia mantiki hii, Rais wa Benki ya Vatican bwana Ernst Von Freyber,
katika mahojiano maalum na Radio Vatican alibainisha kwamba, Benki ya Vatican, kabla
ya kufunga mwaka 2013, inatarajia kufungua tovuti yake itakaotumika kuonesha shughuli
mbali mbali zinazotekelezwa na Benki ya Vatican katika masuala ya fedha pamoja na
kutoa taarifa yake ya Mwaka itakayoonesha shughuli mbali mbali za Benki ya Vatican.
Uongozi
wa Benki ya Vatican unaendelea kuimarisha ushirikiano pamoja na kupokea ushauri na
vigezo vya kimataifa katika kupambana na utakatishaji wa fedha haramu zinazoweza kutumiwa
pia kugharimia vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Ni pale tu ambapo
thamani za jamii na kutete roho ya upendo, kutoa kwa moyo radhi, mshikamano, ustahilivu
na haki vitakapotawala hapo ndipo jamii itakapoweza kujenga hali ya mazingira sahihi
kwa matumizi sahihi ya fedha kwa mafao ya wengi.
Jamii inakumbushwa kwamba,
fedha ina nguvu ya kuokoa, kukomboa, kujenga na kuimarisha upendo sanjari na kusaidia
jitihada za kukuza na kuimarisha utu wa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu. Lakini fedha pia ina nguvu ya kumfanya mwanadamu kuwa mtumwa na pamoja na kuibua
hisia ya kupenda kuwatala wengine; kunyonya na kuwa na matumizi mabaya ya fedha. Fedha
itumike kwa uwajibikaji mkubwa.