Wanachama wa vyama na mashirika ya kitume waadhimisha Mwaka wa Imani mjini Vatican
Kesha la Maadhimisho ya Siku kuu ya Pentekoste kwa mwaka 2013 limekwenda sanjari na
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa kuwashirikisha wanachama wa vyama na mashirika ya
kitume 150, kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Wanachama hawa waliianza siku ya Jumamosi
kwa kutembelea kaburi la Mtakatifu Petro pamoja na kukiri imani yao kwa Kristo na
Kanisa lake, changamoto ya kuendelea kutolea ushuhuda imani hiyo katika uhalisia wa
maisha.
Kesha la Pentekoste limekuwa ni fursa kwa waamini: kusali na kufanya
tafakari ya kina kuhusu Neno la Mungu ambalo limekuwa ni taa na dira inayowaongoza
waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani wakiungana na Khalifa wa Mtakatifu
Petro. Uwepo wa umati mkubwa wa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia ni ushuhuda
wa imani tendaji na changamoto iliyotolewa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Ni
maneno ya Askofu mkuu Rino Fisichella, wakati alipokuwa anamkaribisha Baba Mtakatifu
Francisko ili kuungana na umati mkubwa wa waamini waliokuwa wamemiminika kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na viunga vyake kwa ajili ya kuadhimisha Mwaka wa
Imani, wakitoa ushuhuda wa yale yaliyojiri siku ile walipokutana na Yesu Kristo Mfufuka
kwa mara ya kwanza. Zote hizi ni karama za Roho Mtakatifu ambazo amelijalia Kanisa
katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.
Ni wanachama wa vyama na mashirika ya
kitume yenye karama na mapaji mbali mbali walioamua kuyatumia kwa kushiriki kikamilifu
katika mchakato wa Uinjilishaji kwa ulimwengu mamboleo. Ni waamini wenye ari, uvumilivu
na ujasiri uliowafanya kuweza kuungana na waamini wengine kutoka sehemu mbali mbali
za dunia ili kushirikishana utajiri wa Neno la Mungu na ushuhuda wa imani tendaji.
Wote
hawa anasema Askofu mkuu Fisichella wako tayari kwa ajili ya kutangaza Habari Njema
ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Wanatambua changamoto na magumu wanayokutana nayo
katika maisha na utume wao, lakini kamwe hawezi kukata tamaa, kwani wamekirimiwa nguvu
ya Roho Mtakatifu.