Ushuhuda wa Papa Francisko wakati wa Kesha la Pentekoste kwenye Uwanja wa Kanisa kuu
la Mtakatifu Petro mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Kesha la Sherehe ya Pentekoste alipata fursa ya
kujibu maswali makuu manne ambayo kimsingi yaligusia kwa namna ya pekee Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani: jinsi ambavyo mwamini anavyoweza kuwa na uhakika wa imani yake
kwa Kristo na Kanisa lake.
Dhamana na utume wa vyama na mashirika ya kitume
katika utekelezaji wa changamoto ya Uinjilishaji Mpya, jambo linalopewa msukumo wa
pekee na Mama Kanisa katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia umejikuta ukiendelea kukabiliana
na myumbo wa imani, maadili na utu wema, changamoto ambazo waamini wanapaswa kuzifanyia
kazi katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya maadili na utu wema.
Baba
Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa vyama na mashirika ya kitume waliokuwa
wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika
Kesha la Sherehe ya Pentekoste. Anasema, imani yake inapata chimbuko katika maisha
ya familia yake, iliyobahatika kumfundisha na kumrithisha amana za imani ya Kikristo.
Huu ni mwaliko kwa wazazi na walezi kutekeleza wajibu wao makini katika kuwafundisha
na kuwarithisha watoto wao imani ya Kristo na Kanisa lake.
Baba Mtakatifu anakumbuka
ile tarehe 21 Septemba 1953, alipokuwa na umri wa miaka 17, alipopata nafasi ya kuungama
na kujisikia kutoka katika undani wa moyo wake kwamba, kuna kitu ambacho kimebadilika,
akajisikia kuwa na wito wa kutaka kuwa Padre. Mwenyezi Mungu alimtafuta katika Sakramenti
ya Upatanisho, akamwonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Anawaalika waamini
kujisomea lakini zaidi wajibidishe kukutana na Kristo anayewakirimia na kuwaimarisha
katika safari ya imani.
Anasema, kwa nguvu zao binafsi watashindwa kama ilivyojionesha
kwa Mtakatifu Petro, alipomkana Yesu mara tatu na mara Jogoo akawika. Waamini wajibishe
zaid na zaidi katika maisha ya Kisakramenti kwa kupokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu
pamoja na kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Wasisahau
Tafakari ya Neno la Mungu na kusali kama yalivyokuwa maisha ya Bikira Maria.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Uinjilishaji Mpya ni changamoto endelevu kwa kila
mwamini ili kuweza kuwashirikisha wengine imani kwa Kristo na Kanisa lake. Jambo la
msingi ni kutambua kwamba, chemchemi ya imani ni Kristo mwenyewe. Dhamana hii inatekelezwa
kwa namna ya pekee kwa kujichimbia katika maisha ya sala, kama njia ya kuzungumza
na Mungu pamoja na kumwabudu Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, anayewasubiri
waamini pale kwenye Tabernakulo.
Mwamini akishajichotea nguvu na ari kutoka
kwa Kristo anaweza kumshuhudia katika uhalisia wa maisha yake, wakitoa fursa kwa Kristo
ili aweze kuwapatia dira na mwongozo wa kutekeleza dhamana hii nyeti katika mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ushuhuda wa imani ni njia makini ya kuwashirikisha
wengine imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa amana ya Injili ya Kristo.
Ulimwengu
mamboleo unawahitaji mashahidi wa imani wanaoweza kuzungumza kwa njia ya ushuhuda
wa maisha yao adili mintarafu kweli za Kiinjili. Wakristo wanahamasishwa kutoka katika
ubinafsi wao ili kuwaonjesha wengine imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Baba
Mtakatifu Francisko akijibu swali la tatu kuhusu Kanisa na Maskini, Maadili na utu
wema, anasema, Kanisa halina budi kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu,
kwa kujitahidi kumwilisha Habari Njema ya Wokovu katika uhalisia wa maisha kama njia
ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika: haki, amani, upendo na mshikamano
wa kidugu. Hii ndiyo njia makini ambayo Kanisa linaweza kuwashirikisha wengine kutambua
na kumthamini mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hii inatokana na ukweli
kwamba, athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni matokeo ya kumong'onyoka kwa misingi
ya kimaadili na utu wema. Mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hana tena
kipaumbele cha kwanza katika mipango na mikakati ya uchumi na maendeleo.
Katika
mazingira kama haya, Kanisa linachangamotishwa kutoka katika undani wake na kuwaendea
wale wanaoishi pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha, ili kuwaonjesha
upendo na huruma ya Mungu. Ni mwaliko wa kumfungulia mlango Kristo ili aweze kupata
nafasi katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu.
Kanisa halina budi kuanzisha
na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na kuwashirikisha
wote kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu bila kupoteza utambulisho wao kama
wafuasi wa Kristo.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Maskini hawana
budi kupewa kipaumbele cha pekee, kwa kuheshimu na kuthamini utu wao; kwa kuwasaidia
kupambana na njaa, umaskini na magonjwa, kwani wote hawa ni sehemu ya Fumbo la Mwili
wa Kristo. Maskini wanawafundisha waamini ule upendo wa Mungu unaojionesha katika
Fumbo la Umwilisho, changamoto kwa waamini kutopenda mno malimwengu, kwani huko wanaweza
kutopea na kuchanganyikiwa!
Kimsingi, myumbo wa uchumi kimataifa unagusa undani
wa mtu mzima. Ni mwaliko wa kusimama kidete katika misingi ya maadili na utu wema,
kwani kumong'onyoka kwa maadili kuna madhara makubwa katika maisha na maendeleo ya
watu. Mchakato wa uwekezaji katika taasisi za fedha uzingatie utu na heshima ya mwanadamu,
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Jumuiya ya Kimataifa ifanye jitihada
za makusudi ili kuokoa maisha ya watu badala ya kujielekeza zaidi katika Mabenki.
Kanisa kwa upande wake, linapaswa kutolea ushuhuda wa upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii.
Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali la nne na la mwisho
anasema kwamba, waamini wanachangamotishwa kutembea, kulijenga Kanisa na kumshuhudia
Kristo kama njia makini ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa
ujasiri na moyo mkuu. Kuna mashahidi wa Kanisa la Mwanzo walioyamimina maisha yao
kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hii ndiyo njia ambayo wanaionesha wakristo wanaokabiliana
na madhulumu ya kidini kama ilivyo nchini Pakistan. Wakristo hawa wanatoa sadaka ya
maisha yao kwa ajili ya Kristo.
Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwamba, wakati
mwingine vurugu na madhulumu ya kidini yanafumbata sababu mbali mbali ambazo zinajionesha
katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Dini inatumika kama "danganya toto".
Huu ni mwaliko kwa Wakristo kushinda ubaya kwa kutenda wema, jambo ambalo wakati mwingine
si rahisi, kwani hapa yataka moyo!
Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia
wote wanaodhulumiwa kutokana na dini zao, kutambua kwamba, yuko pamoja nao. Anawaalika
Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, kuwasindikiza kwa sala na mshikamano wa kidugu.
Viongozi wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa wahakikishe kwamba, uhuru wa
kidini unaheshimiwa na kuthaminiwa. Kila mtu apewe fursa ya kukiri na kutolea ushuhuda
wa imani yake, kwani kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu
anawataka waamini kufungua malango ya matumaini na kamwe wasijifungie ndani, bali
wawe tayari kujitosa kuwaendea wote wanaoishi na kusukumizwa pembezoni mwa Jamii.