2013-05-19 10:35:58

"Nimeng'atuka kwa ajili ya mafao na ustawi wa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Songea"


Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni aliridhia Ombi lililotolewa na Askofu mkuu Norbert Wendelin Mtega wa Jimbo kuu la Songea, Tanzania kutaka kung'atuka kutoka madarakani. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania likafafanua kwamba, hii ni kutokana na sababu za afya ambazo zimemsukuma Askofu mkuu Mtega kung'atuka kutoka madarakani.

Hivi karibuni, Askofu mkuu mstaafu Mtega alizungumza na waandishi wa habari akikazia kwamba, ameamua kung'atuka kutoka madarakani kutokana na sababu za afya kuanza kuleta mgogoro na hivyo kumnyima fursa ya kuweza kuwahudumia kwa ukamilifu waamini wa Jimbo kuu la Songea. Anasema, amekuwa akisumbuliwa na magonjwa mbali mbali, ikiwa ni pamoja na shinikizo la damu, miguu na magoti kujaa maji, kukosa usingizi kwa muda mrefu na hali ya kusikia kizungu zungu, jambo ambalo limempekea kuanguka mara kadhaa.

Anasema hizi ni dalili za hatari na kwamba, haya yalikuwa ni matatizo makubwa ya afya ambayo yanamnyima fursa ya kutekeleza wajibu wake barabara wa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, Jimbo kuu la Songea. Kutokana na sababu hizi msingi kwa hiyari na utashi wake kamili akaamua kumwomba Baba Mtakatifu Francisko aliangalie jambo hili pamoja na kumpatia nafasi ya kumtafuta Askofu mkuu mwingine atakayeendeleza kazi ya Kristo, Jimbo kuu la Songea. hakupenda kung'ang'ania madarakani kwani hasara zake zingekuwa kubwa kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Songea.

Anaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu amjalie afya na maisha ili aendelee kuchangia katika ustawi na maendeleo ya watanzania hata katika awamu hii ya maisha yake. Amewataka watanzania kushikamana kwa dhati ili kujenga na kudumisha umoja, upendo, haki na amani bila kuendekeza ukabila na udini, mambo ambayo kimsingi ni sumu ya maendeleo ya binadamu.

Anasema, Kanisa bado linakabiliwa na changamoto ya kuwaendeleza watanzania katika nyanja mbali mbali za maisha, lakini zaidi katika sekta ya elimu, afya, maji na utunzaji bora wa mazingira. Kanisa halina budi kuendeleza mchakato wa kujitegemea na kuwategemeza waamini wake.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Norbert Wendelin Mtega amekuwa ni Askofu kwa kipindi cha miaka 28, kati ya miaka hii, ametumia miaka 6 kuliongoza Jimbo Katoliki la Iringa na miaka 22 amekuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Songea. Kwa miaka mingi amekuwa ni Mwenyekiti wa Idara ya Elimu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na mafanikio yake yanaonekana kwa kuzaliwa kwa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania kinachoendelea kutamba kwa huduma na ubora wa elimu nchini Tanzania.

Askofu mkuu mstaafu Norebert Mtega ameshiriki mara kadhaa katika Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu na mara ya mwisho alichaguliwa kuwa ni kati ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.