Kanisa linasali kwa ajili ya Familia ya Mungu duniani
Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2013 yameongozwa na kauli mbiu “Mimi
nina amini niongezee imani” . Waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia walishiriki
pia katika Sala za Waamini, ambazo kwa namna ya pekee, waamini wamemwomba Roho Mtakatifu
ili aweze kulidumisha Kanisa katika umoja unaobubujika kutoka katika Sadaka ya Kristo
Msalabani na umoja huu uweze kuenea miongoni mwa watu wa Mataifa.
Pentekoste
ni Siku kuu ya Waamini walei na Kanisa limewaombea wanachama wa vyama na mashirika
ya kitume ili kwa kusaidiwa na Roho Mtakatifu waoneshe ile sura ya Kristo pamoja na
kuwakirimia uwezo wa kushuhudia imani yao kwa nguvu na upendo unaokoa.
Kanisa
linatambua kwamba, bado kuna wadhambi, wenye mashaka na wasioamini. Wote hawa wameombewa
ili Roho Mtakatifu aweze kuifungua mioyo yao kusikiliza na kuitii Injili inayowawezesha
kumfahamu Bwana Yesu Kristo.
Mama Kanisa anawajali na kuwathamini vijana wa
kizazi kipya. Hawa wameombewa ili waweze kuwa waaminifu katika urafiki wao na Yesu
Kristo anaye wachangamotisha kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Roho Mtakatifu awawezeshe
kufanya maamuzi ya kishujaa.
Mwishoni, Kanisa limesali na kumwomba Roho Mtakatifu
awaangazie viongozi wa Serikali na watu wenye mapenzi mema, ili macho yao yaone mahitaji
msingi ya ndugu zao, hatimaye waweze kujielekeza kufanya maamuzi bora kwa mafao ya
wengi, haki na amani. Sala kwa lugha ya Kiswahili imetolewa na Dr. James Msekela,
Balozi wa Tanzania nchini Italia.
Itakumbukwa kwamba, waamini wanaoshiriki
katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wanaweza
kupata Rehema Kamili, ikiwa kama watafuata masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa. Yaani,
kutokuwa na doa la dhambi ya mauti au dhambi ndogo. Kupokea Sakramenti ya Kitubio
na Ekaristi Takatifu pamoja na kusali kwa nia za Baba Mtakatifu Francisko.