2013-05-19 11:45:44

Jubilee ya miaka 25 ya huduma kwa Maskini Mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 21 Mei 2013 anatarajiwa kuwatembelea Masista Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Masista wa Mama Theresa wa Calcutta, katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 tangu Nyumba ya Zawadi ya Maria ilipoanzishwa mjini Vatican kwa utashi wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, ili kutoa huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Nyumba hii ilifunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kunako tarehe 21 Mei 1988. Tangu wakati huo, kila siku Watawa wanatoa chakula kwa maskini wanaobisha hodi katika nyumba hii. Hapa wanahifadhiwa pia wasichana na wanawake wasiokuwa na makazi maalum bila kuzisahau familia ambazo zinakabiliana na hali ngumu ya maisha. Uwepo wa nyumba hii ni kielelezo cha upendo na mshikamano wa Mama Kanisa kwa maskini na wahitaji zaidi.

Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kutoa changamoto kwa Kanisa kuonesha upendeleo wa pekee kwa maskini, atakutana na kuzungumza na watawa na wale wanaohudumiwa nyumbani hapo. Itakumbukwa kwamba, nyumba hii imetembelewa mara kadhaa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita na sasa anakwenda huko Papa Francisko.







All the contents on this site are copyrighted ©.