Sensa ya watu na makazi inafanyika kwa mara ya kwanza nchini Angola tangu ilipojipatia
uhuru wake! Inagharimiwa na Angola yenyewe!
Nchi ya Angola, kwa mara ya kwanza imeanza kufanya sensa ya watu na makazi tangu ilipojipatia
uhuru wake. Mara ya mwisho Angola ilifanya sensa ya watu na makazi kunako mwaka 1973
miaka miwili kabla ya kujipatia uhuru wa bendera, lakini baada ya muda mfupi, Angola
ilijikuta ikingia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo kwa takribani miaka ishirini
imekuwa ni kikwazo kikubwa cha ustawi na maendeleo ya wananchi wa Angola.
Umoja
wa Mataifa, Brazil, Cape Verde na Msumbiji zitatoa msaada wa kiufundi ili kufanikisha
zoezi hili. Serikali ya Angola inakadiria kwamba, gharama ya sensa na makazi ya watu
nchini humo itagharimu kiasi cha dolla za kimarekani Millioni 73 sawa na kiasi cha
Billioni 7 za Kwanza ambayo ni fedha ya Angola.
Hayo yamebainishwa na Bwana
Camilo Ceita, Mkurugenzi wa Taasisi ya Takwimu nchini Angola na kukazia kwamba, Angola
ni kati ya nchi chache sana Barani Afrika ambazo zinaendesha sensa ya watu na makazi
kwa kutumia fedha yake bila kuhitaji msaada wa wafadhili kutoka nje ya nchi.