Mapadre na Watawa hawaruhusiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa!
Baraza la Maaskofu Katoliki DRC limetoa mwongozo unaowakataza Mapadre na Watawa kugombea
nafasi za uongozi kwenye Tume ya Huru ya Uchaguzi nchini DRC. Tume hii ina wajibu
wa kuratibu mchakato wote wa uchaguzi kuwa unafanyika katika haki na uhuru kamili.
Kwa sasa vyama mbali mbali vya kisiasa na vile vya kiraia vinajipanga kuhakikisha
kwamba, vinakuwa na uwakilishi katika Tume Huru ya Uchaguzi nchini DRC kadiri ya sheria
iliyotungwa na kupitishwa na Bunge hivi karibuni.
Padre Fèlicien Mwanama, Katibu
mkuu msaidizi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anasema,
kadiri ya sheria za Kanisa Mapadre na Watawa hawaruhusiwi kujihusisha na masuala ya
kisiasa. Sheria zinafafanua kwamba, Askofu mahalia anaweza kutoa kibali kwa Padre
au Mtawa kujiunga na shughuli za kisiasa kwa sababu maalum.
Tume Huru ya Uchaguzi
DRC itaundwa na kundi la watu kumi na tatu: sita watachaguliwa kutoka katika Chama
Tawala na wajumbe wanne watachaguliwa kutoka katika vyama vya upinzani na watatu,
hawa watachaguliwa kutoka katika vyama vya kiraia. Katiba ya DRC inaonesha kwamba,
Tume hii itakuwa chini ya Mwenyekiti na wengine ni wajumbe watakaoshiriki katika utekelezaji
wa shughuli na maamuzi ya kila siku na kwamba, inatakiwa kutekeleza majukumu yake
bila kuingiliwa na wanasiasa wala Serikali.
Hivi karibuni, Baraza la Maaskofu
DRC liliitaka Serikali na vyama vya kisiasa nchini humo kuanzisha mchakato wa majadiliano
ya kitaifa unaopania kuponya madonda ya kinzani na utengano; mambo ambayo yamechangia
kukosekana kwa amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa. Rasilimali na utajiri wa nchi
utumike kwa mafao ya wengi badala ya kuendelea kuwanufaisha wajanja wachache ndani
ya Jamii. Kuna haja pia ya kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo kwa kuondokana
na kilimo cha jembe la mkono, ili kuongeza tija na pato kwa wakulima hasa wale wanaoishi
vijijini.
Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linasikitishwa na hali ya umaskini
wa hali na kipato unaowakumba wananchi wengi kwa sasa. Ili haki, amani na utulivu
viweze kupatikana na kudumishwa, kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa katika: Mahakama
na Jeshi la Polisi na pamoja na Vikosi vya Ulinzi na Usalama; kama dawa ya kupambana
na ufisadi, rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma; mambo ambayo pia yamechangia kuporomoka
kwa amani nchini DRC.