2013-05-18 08:24:33

Biashara haramu ya binadamu inaendelea kushamiri duniani!


Tathmini ya Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na biashara haramu ya binadamu uliozinduliwa kunako mwaka 2010 imekuwa ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kusimama kidete kupinga kwa nguvu zote biashara haramu ya binadamu inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Ni fursa ya kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha kwamba, utumwa na aina zote za nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu zinatoweka katika uso wa dunia. Waathirika hawana budi kusaidiwa ili kuanza tena mchakato wa maisha yao ya kawaida.

Ni mchango wa Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa alipokuwa anachangia hoja kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokuwa linajadili kuhusu biashara haramu ya binadamu. Anasema, haitoshi kwa Jumuiya ya Kimataifa kulaani biashara hii, bali Serikali zinapaswa kuonesha utashi wa kisiasa kwa kutekeleza maamuzi mbali mbali yanayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa. Hii inatokana na ukweli kwamba, leo hii tatizo la uhamiaji ni sehemu ya maisha ya Jumuiya ya Kimataifa halina majadala.

Baadhi ya watu wanatumia tatizo la uhamiaji kama mwanya wa kuendeleza biashara haramu ya binadamu, hali inayochangia kukua na kuongezeka kwa vitendo vya jinai ulimwenguni. Biashara hii inadhalilisha utu na heshima ya binadamu na ni kikwazo kikubwa cha ushirikiano na mshikamano wa kimataifa. Kamwe, watu wasitumiwe kama biashara, ili kukidhi uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka kwa baadhi ya watu ndani ya Jamii.

Sheria hazina budi kutumika ili kudhibiti wimbi la biashara haramu ya binadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, waathirika wa biashara hii wanahudumiwa vyema. Ili kufanikisha azma hii kuna haja ya kuchangia kwenye Mfuko wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa biashara haramu ya binadamu. Itakumbukwa kwamba, waathirika wakuu ni wanawake na watoto.

Askofu mkuu Chullikatt anabainisha kwamba: sera makini, masuala ya kijamii na sheria ni mambo muhimu katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, lakini hata Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya upembuzi yakinifu utakaoweka wazi sababu na mazingira yanayopelekea baadhi ya watu kutumbukia na kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu. Kutokana na umaskini na uduni wa maisha, baadhi ya wanawake na wasichana wamejikuta wakitumbukia kwenye utumwa mamboleo. Wanawake wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na kamwe wasitumike kama vichokoo vya matangazo ya biashara.

Biashara ya ngono duniani inachangia asilimia 58% ya nyanyaso za ngono, hali inayoonesha kwamba, utumwa mamboleo unazidi kukua na kupanuka siku hadi siku, jambo linalohitaji kuwekewa mikakati makini ili kudhibiti na hatimaye, kukomesha biashara hii ambayo imeendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Tatizo hili linajionesha pia katika haki za wafanyakazi sehemu mbali mbali za dunia, hali inayodhalilisha pia maana na thamani ya kazi katika maisha ya mwanadamu.

Askofu mkuu Chullikatt anasema kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kukazia umuhimu wa maadili na utu wa mwanadamu katika maeneo ya kazi, sanjari na kuheshimu haki msingi za binadamu. Ni umaskini wa hali, kipato pamoja na mmong'onyoko wa kimaadili unaopelekea baadhi ya watu kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu.

Ni watu wanaotamani wakati mwingine kusaidia maboresho ya maisha ya familia zao, lakini kwa bahati mbaya wanaangukia mikononi mwa wanyonyaji na wadhulumati. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika mapambano dhidi ya baa la njaa pamoja na kujenga mazingira yatakayosaidia maboresho ya uchumi, ili kutoa fursa zaidi kwa watu kuboresha hali yao ya maisha. Umaskini wa kipato unapelekea watu wengi kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu. Watu waheshimiwe, walindwe na kuthaminiwa na kamwe wasigeuzwe kuwa ni biadhaa.

Askofu mkuu Francis Chullikatt anafafanua kwamba, Kanisa Katoliki kwa kutumia: Taasisi na Mashirika yake ya misaada kimataifa na kitaifa limeendelea kuwasaidia wahanga wa biashara haramu ya binadamu kwa hali na mali. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujifunga kibwebwe kupambana kufa na kupona ili kutokomeza biashara haramu ya binadamu sanjari na kujenga upendo na mshikamano wa kidugu.







All the contents on this site are copyrighted ©.