Bi Angela Merkel akutana na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 18 Mei 2013 amekutana na kuzungumza na
Chancellor wa Shirikisho la Ujerumani Bi Angela Merkel. Baadaye, alikutana na kuzungumza
na Askofu mkuu Domique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.
Katika
mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Bi Angela Merkel, wamegusia uhusiano
uliopo kati ya Ujerumani na Vatican. Wamepembua hali ya: kijamii, kiuchumi, kisiasa
na kidini Barani Ulaya na duniani katika ujumla wake. Viongozi hao wamekazia kwa namna
ya pekee, umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Kuna
haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kukomesha vitendo vya madhulumu dhidi ya wakristo kwa
kukazia uhuru wa kidini pamoja na ushirikiano wa kimataifa unaopania kujenga na kudumisha
amani.
Viongozi hawa wameangalia pia tunu msingi za maisha ya Jumuiya ya Ulaya,
uwajibikaji duniani kwa kusema kwamba, kuna haja ya kwa viongozi wa Serikali na Kidini
kutekeleza wajibu wao kama kikolezo cha maendeleo endelevu yanayojengeka katika msingi
wa utu, heshima ya binadamu pamoja na mshikamano unaoongozwa na kanuni ya auni.