Barua ya wazi kutoka SECAM kuhusu Ukwepaji wa kodi
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM limeandika
barua ya wazi kwa wajumbe wa Mkutano wa Kodi Barani Ulaya utakaofanyika hapo tarehe
22 Mei 2013 kuangalia uwezekano wa kuwa na sera na sheria makini zitakazowabana wakwepa
kodi wanaokwamisha juhudi za watu kujiletea maendeleo yao wenyewe.
Hili ni
kundi ambalo limeendelea kujinufaisha kwa kujipatia pato kubwa lisilo halali kutokana
na kukwepa kulipa kodi katika nchi husika, lakini hali ni mbaya zaidi kwa nchi maskini
duniani.
Askofu Gabriel Mbilingi, Makamu wa Rais, SECAM anasema, wamepokea
kwa mikono miwili uamuzi uliofanywa na Umoja wa Ulaya wa kuitisha mkutano wa Kodi
Barani Ulaya, juhudi ambazo zinapaswa kwenda sanjari na utashi wa kisiasa wa kutekeleza
maamuzi magumu kwa ajili ya mafao ya Jamii husika. Kila mwaka kuna mammillioni ya
fedha yanatoweka, kwa njia ya kukwepa kulipa kodi na matokeo yake Serikali zinakosa
mapato au zinapata "kiduchu" ikilinganishwa na kodi halali iliyopaswa kutolewa.
Takwimu
za kuaminika kutoka katika taasisi za Fedha Kimataifa, "Global Financial Instutions"
zinaonesha kwamba, kila mwaka Dolla za Kimarekani millioni 725 hadi millioni 810
zinatoroshwa kutoka katika nchi maskini zaidi duniani. Kiasi hiki cha fedha ni kikubwa
kwani kinahitajika kwa ajili ya kuwekeza katika maboresho ya hali ya maisha ya wananchi
wanaoishi katika Nchi zinazoendelea. Ukwepaji wa kodi ni ukiukwaji wa haki, jambo
ambalo halina budi kufanyiwa marekebisho ya haraka na taasisi za fedha kimataifa na
kitaifa.
Askofu mkuu Mbilingi anawaambia wajumbe wa mkutano wa kodi Barani
Ulaya kutambua kwamba, wanayo dhamana nyeti ya kimaadili na kisiasa kufanya mabadiliko
haya yanayohitajika kwa sasa, ili kujenga na kuimarisha mshikamano wa kidugu kwa kupunguza
anasa, ili fedha hizi zisaidie katika mchakato wa kuwaletea wananchi maendeleo endelevu
pamoja na kuenzi amani na utulivu. Ni matumaini ya SECAM kwamba, Bwana Herman Van
Rompuy, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, watalishughulikia tatizo hili kwa uwajibikaji
utakaojionesha katika matendo kwa nchi za Ulaya na katika Jumuiya ya Kimataifa.
SECAM
inashauri kwamba, kuwepo na viwango vya kimataifa kuhusiana na ubadilishanaji wa habari
na takwimu za fedha katika hali ya uwazi ili mamlaka za kodi na mapato ziweze kutoza
kodi stahiki. Kuna haja ya kuendelea kufanya maboresho kwa kuzingatia ukweli na uwazi
katika masuala ya fedha kimataifa na kitaifa ili kuwawajibisha wahusika katika masuala
ya kodi.
Makampuni ya kimataifa hayana budi kutekeleza mitaji yake kwa kuzingatia
ukweli na uwazi. Sheria zilizopo ziimarishwe na kuborshwa ili kuwabana wakwepa kodi
na kwamba, kila upande unapaswa kutekeleza wajibu wake kwa njia ya haki pamoja na
kutafuta mafao ya wengi.