Wito na utume wa Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu
Mheshimiwa Sr. Maria Eugenia Thomas, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Kazi ya Roho
Mtakatifu katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha kwamba, wao kama Shirika wana
utume wa kuendeleza kazi ya Yesu Kristo Mfufuka aliyemtuma Roho Mtakatifu ili kuendeleza
ile kazi iliyokuwa imeanzishwa na Yesu kwa kuwakumbusha waamini yale yaliyofundishwa
na Yesu pamoja na kuwafunulia ukweli wote.
Kama Masista
wa Kazi ya Roho Mtakatifu wanatumwa kupeleka upendo wa Mungu aliyejifanya mwanadamu,
hivyo wanapaswa kusikiliza kwa makini na kufuata maongozi ya Roho Mtakatifu, ili kusoma
alama za nyakati na kutenda kadiri ya mahitaji ya watu wa nyakati hizi. Lengo ni kupata
Pentekoste Mpya ambayo Mwenyezi Mungu atakuwa yote katika yote. Hii inamaanisha kuleta
mabadiliko katika maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Hii ni changamoto
kwa kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kushiriki katika mchakato unaopania
kumletea mwanadamu maendeleo endelevu kwa kusoma alama za nyakati sanjari na utunzaji
wa mazingira na mafao ya wengi. Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu wanatumwa kuwa ni
vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano kama sehemu ya mchakato wa kumwendeleza
mtu mzima.