Watu wanasubiri kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa na wahudumu wanaoshuhudia
furaha ya Injili kwa kujitoa bila ya kujibakiza!
Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wakurugenzi wa kitaifa wa Mashirika
ya Kipapa ya kazi za kimissionari kwa kumsaidia katika utume wa Uinjilishaji hadi
miisho ya dunia. Mashirika haya ni chombo mahususi mikononi mwa Khalifa wa Mtakatifu
petro ambaye kimsingi ni kielelezo cha umoja na Ukatoliki wa Kanisa.
Ni Mashirika
ya Kipapa kwani yanatekeleza utume wake kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili
amana ya Injili iweze kuwafikia wengi na kwamba, kuna idadi kubwa ya watu ulimwenguni
ambao wana kiu ya kutaka kusikiliza Injili ya Kristo, changamoto kwa wadau kupambanua
mbinu na njia mpya za kuweza kulifikisha Neno la Mungu katika mioyo ya watu, ili kuwashirikisha
zawadi ya imani ili hatimaye, iweze kuwa ni mwanga katika njia ya maisha ya waamini.
Baba
Mtakatifu Francisko ameyasema hayo Ijumaa, tarehe 17 Mei 2013 alipokuwa anazungumza
na Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari waliokuwa wanafanya
mkutano wao mkuu wa Mwaka hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, utume
huu ni mgumu, lakini kwa njia ya maongozi ya Roho Mtakatifu unapata mwuto mkubwa zaidi.
Mwanadamu katika hija ya maisha yake anakabiliana na udhaifu wa aina mbali mbali,
lakini Injili ya Kristo haina budi kutangazwa hadi miisho ya dunia.
Waamini
watambue kwamba, nguvu ya Uinjilishaji inatoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, wanaalikwa
kufungua mioyo yao ili Roho Mtakatifu awasaidie kujitoa na kuwa ni vyombo vya huruma,
wema na upendo wa Mungu kwa kila mtu, lakini zaidi kwa wale wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii. Huu ni utume unaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na kila mwamini pamoja
na Kanisa katika ujumla wake, kwani wokovu wa Mungu ni kwa kila mwanadamu.
Baba
Mtakatifu anawaalika Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari kutambua
kwamba, utume wao una chapa ya Ukatoliki, wenye heshima, wajibu na dhamana ya kuendeleza
kazi ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwasaidia wahitaji. Ni mwaliko
wa kuanza kukuza na kulea moyo na ari ya kimissionari miongoni mwa Wakristo tangu
wakiwa bado na umri mdogo pamoja na kuendelea kuchangia na kuhamasisha moyo wa kimissionari
kila mtu kadiri ya nafasi yake.
Viongozi hawa walisaidie Kanisa kutekeleza
utume wake wa Uinjilishaji kwa kushirikiana na Maaskofu mahalia, ili kujenga na kuimarisha
moyo wa kimissionari, umoja na ushirikiano na Makanisa mahalia kwa ajili ya kutangaza
Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia.
Ni wajibu wao kutangaza na kushuhudia
unabii na utume wa Kanisa katika Uinjilishaji, kwa kuendelea kutoa kipaumbele cha
pekee kwa Makanisa machanga zaidi duniani, yanayoendelea kutekeleza dhamana hii katika
mazingira magumu, ubaguzi na madhulumu; ili yaweze kuimarishwa na kusaidiwa na ushuhuda
wa maneno na kazi za Kiinjili.
Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, amewataka
Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari kushiriki kwa kutekeleza
wajibu wao kwa Kanisa la kiulimwengu, ili watu wote waweze kusikia Habari Njema ya
Wokovu.
Kwa maombezi ya Bikira Maria nyota ya Uinjilishaji Mpya, watu wanaoishi
katika ulimwengu mamboleo, wanaoendelea kuogelea katika wasi wasi, wapate matumaini
na Habari Njema ya Wokovu kutoka kwa Wahudumu wa Injili wanaoshuhudia kwa furaha Injili
ya Kristo waliyoipokea kwa kujitoa bila ya kujibakiza, ili kutangaza Injili na kulisimika
Kanisa ulimwenguni.