Ujumbe wa Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2013 kutoka kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni
Basi yeye, akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu, na kupokea kwa Baba ile
ahadi ya Roho Mtakatifu, amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisia. Ni sehemu
ya Neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume ambayo ni kauli mbiu inayoongoza
ujumbe wa Siku kuu ya Pentekoste kutoka kwa Marais wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni
kwa mwaka 2013.
Katika kipindi
cha Pasaka, waamini wamepata fursa ya kusherehekea ufufuko na hatimaye, kupaa kwa
Bwana Yesu Kristo mbinguni. Kanisa kwa sasa linaadhimisha Sherehe ya Pentekoste, siku
ile ambayo Mwenyezi Mungu aliukirimia ulimwengu zawadi ya Roho Mtakatifu, changamoto
kwa waamini kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo sanjari na kuwatumikia
jirani zao ambao bado hawajabahatika kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa masikioni
mwao kwamba, kwa hakika Yesu anawapenda.
Itakumbukwa kwamba, hata kabla ya
Wakristo wa kwanza kuadhimisha Sherehe hii, Wayahudi walikuwa wanaisherehekea kwa
kama Siku kuu ya Mavuno, kwa kumtolea Mwenyezi Mungu mavuno ya kwanza. Walikumbuka
jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani Misri pamoja na kuwapatia
Amri kumi, dira na utambulisho wao kama taifa teule la Mungu. Miaka mingi imekwisha
yoyoma tangu Waisraeli walipoadhimisha Sherehe ya Pentekoste, wakikumbuka kazi ya
ukombozi iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu.
Leo hii Pentekoste imepata sura
na maana mpya. Waamini hawalazimiki tena kumtolea Mwenyezi Mungu mavuno ya kwanza
na kinyume chake ni kwamba, Mwenyezi Mungu anawakirimia waamini zawadi ya Roho Mtakatifu
anayewasha mioyo ya waamini kwa upendo wa Kimungu kwa kuonesha kutoka kwa Kristo Mfufuka
wokovu wa ulimwengu.
Katika miaka ya hivi karibuni watu wengi wameendelea kukabiliana
na changamoto mbali mbali: kifedha na kiroho hali inayotishia amani na usalama wa
dunia. Ujio wa Roho Mtakatifu uamshe tena moyo n aari ya kiekumene, ili waamini waweze
kujikita kutafuta umoja na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Waamini na
watu wote wenye mapenzi mema washikamane kwa njia ya sala, kwa kujikatalia ili kutenda
haki na kutembea katika njia ya Mungu. Hivi ndivyo Baraza la Makanisa kutoka Pacific
limetafakari wakati wa Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Baraza hili lilipoanzishwa
kutoka Pacific.
Marais wa Mabaraza ya Makanisa Ulimwenguni, wanawaombea waamini
ili waweze kuendeleza hija ya maisha na utume wao huko Pacific, kwa kutolea ushuhuda
wwa upendo wa Mungu usiokuwa na kifani kwa waja wake. Kwa upande wa Baraza la Makanisa
Ulimwenguni, hiki pia ni kiini cha furaha ya ushuhuda wa uwepo wa Roho Mtakatifu
ulimwenguni. Huu ni mwaka ambamo Mabaraza ya Kiekumene Kikanda yanaadhimisha Mikutano
yao mikuu.
Kanisa linawaombea wale watakaofanya mikutano yao Barani Afrika,
Amerika ya Kusini na Ulaya. Baada ya Maadhimisho haya, Makanisa yote yatafanya hija
ya maisha ya kiroho ili kwa pamoja waweze kushiriki Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa
Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa mwaka 2013 utakaofanyika huko Busan, Korea ya Kusini,
wakiongozwa na kauli mbiu ”Mungu wa maisha: tuongoze katika haki na ukweli”.
Marais
wanawaalika waamini wanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kumfungulia nafsi
zao Roho Mtakatifu ili waweze kimarishwa katika utekelezaji wa kufanya kazi pamoja
kwa ajili ya haki ulimwenguni; haki ambayo ni njema; kwa kuendelea kutunza kazi ya
uumbaji pamoja na kuleta amani pale ambapo kuna magomvi, chuki, misigano na vita.
Pentekoste iwe ni fursa kwa waamini kusali kwa ajili ya kuombea amani ambayo
inahitajika sana ulimwenguni. Wanaombea ili Roho Mtakatifu aweze kuleta mabadiliko
katika mioyo ya wote watakaohudhuria mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni
utakaofanyika huko Busan, Korea ya Kusini.