Ni siku nyingine tena tunapokutana katika meza ya Neno la Mungu. Leo tunaadhimisha
sherehe ya Pentekoste, sherehe ambayo katika kalenda ya litrujia huja siku hamsini
baada ya Pasaka.
Ni sherehe
ambayo Wakristo humshangilia Kristo mfufuka katika Roho Mtakatifu na kufurahia ukombozi
ambao umeletwa na Kristo mwenyewe. Katika sherehe ya Pentekoste fumbo la Pasaka hukamilika
maana ni katika sikukuu hii Roho Mtakatifu hulishukia Kanisa ili likaendeleze kazi
ya Kristu bila woga, likiwa na nguvu za kimungu.
Ni Sherehe ambayo kwayo Roho
Mtakatifu huthibitisha muungano wetu na Mungu. Ujumbe wa Neno la Mungu unalala katika
Roho Mtakatifu kuwa sheria mpya na nguvu ya Wakristu, taifa jipya la Mungu lililoshikamana
katika upendo na Mungu.
Katika somo la kwanza toka kitabu cha Matendo ya Mitume,
tunaona Mitume wakiwa mahali pamoja na ghafla upepo na uvumi , ndimi za moto zinawashukia.
Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu na kuanza kunena kwa lugha mbalimbali. Wanapokea
nguvu ya Mungu na hivi wanaweza kutenda matendo ya ajabu kwa mataifa.
Tunasikia
pia, watu waliwashangaa Mitume kwa kuwa watu hawa waliweza kusikia na kuelewa ujumbe
uliokuwa ukihubiriwa na Mitume katika lugha zao. Hii ni ajabu maana baada ya mnara
wa Babeli (Mw.11:1-9) watu hawakuweza kuelewana kiurahisi. Kumbe Roho Mtakatifu ni
muunganishi wa taifa jipya la Mungu ambalo ni tunda la ufufuko.
Ishara mbalimbali
tulizozisikia hapo juu zatupa mwanga ili kuweza kuelewa vema tendo la kushuka kwa
Roho Mtakatifu. Uvumi wa upepo na ndimi za moto zinatupa mazingira ya sheria ya zamani,
yaani wakati sheria ya zamani ilipokuwa ikitangazwa tunaposoma katika kitabu cha kutoka
kulitokea alama hizo. (Kut.19:16). Wakati Musa alipokuwa akipokea sheria ya Mungu
maneno ya Mungu yalibadilika na kueleweka katika ndimi sabini za moto. (Kut.20:18)
Hili lilimaanisha kuwa sheria hii ni kwa ajili ya watu wote duniani. Mwinjili Luka
anapoandika jambo la kushuka kwa Roho Mtakatifu anatumia alama zilezile ili aweze
kueleweka kwa urahisi kwa walengwa wa Neno la Mungu.
Mtakatifu Luka anatumia
alama ya lugha nyingi akionesha utamaduni uliokwishajengeka katika Kanisa la mwanzo,
yaani watu walipompokea Roho Mtakatifu walinena kwa maneno mapya wakimsifu Mungu.
Alama hii ni kielelezo cha umoja wa Kanisa, yaani kanisa lililo kwa ajili ya wokovu
wa wote. Injili ni kwa ajili ya mataifa yote, inatupilia mbali mipaka ya rangi, kijiografia,
lugha na mambo yote yawekayo kando umoja wa taifa la Mungu. Ni kwa njia ya pentekoste
wale wote waliotawanyika wanakusanywa tena kwa sheria mpya yaani sheria ya mapendo
inayounda familia mpya ya Mungu. Sheria hii inaandikwa mioyoni mwa watu
Mtakatifu
Paulo anapowaandikia Wakorinto anawakumbusha kuwa karama walizopewa si kwa ajili ya
ubinafsi bali kwa ajili ya umoja. Anawaambia kuwa Roho ni mmoja na karama ni mbalimbali
kwa ajili ya shughuli za misioni, kwa ajili ya kupamba upendo uleule. Anawakumbusha
hilo akitumia alama ya mwili mmoja ulio na viungo mbalimbali vyenye shughuli mbalimbali
kwa ajili ya mwili mmoja.
Mwishoni, anataka karama ziwe ni chanzo cha mapendo
katika familia yao ndiyo kanisa. Hivi leo katika jamii mbalimbali kuna machafuko kwa
sababu ya kila mmoja kuona karama aliyonayo ni kwa ajili yake mwenyewe na si kwa ajili
ya jumuiya yake. Yafaa kuepuka shida hii mapema ili jumuiya yetu ikae kwa amani.
Katika
somo la injili mwinjili Yohane anatangaza amani ya Kristu ambayo ni zawadi ya ufufuko
na ni msingi wa umisionari. Si tu hilo bali pia ni msingi wa upatanisho na furaha
katika familia ya Mungu maana baada ya kuwapatieni amani atawatuma ulimwenguni kwa
ajili ya kazi ya kitume.
Katika utume Mitume wanaalikwa kuwaondolea watu dhambi
zao. Hawewezi kuondolea dhambi bila Roho wa Mungu na hivi kabla anawavuvia Roho huyo.
Kumbe mpendwa msikilizaji wa radio Vatican, kushuka kwa Roho Mtakatifu ni nguvu ya
ondoleo la dhambi ni amani na furaha ya taifa la Mungu, ni mkazo wa umisionari kazi
ya Kristu.
Roho Mtakatifu anashuka kwa ajili ya kubadili maisha yetu yawe maisha
mapya, yawe ni maisha kwa ajili ya kuwafariji walio katika taabu mbalimbali. Basi
ni wajibu wetu sisi tuliompokea kwa njia ya Sakramenti kuweka maisha yetu kama kielelezo
cha maisha mapya, maisha yampendezayo Mungu na watu. Tukishampokea Roho Mtakatifu
hatutaweza tena kuangalia mambo ya chini bali yaliyo ya juu. Ndiyo kusema Roho wa
Bwana akishaujaza ulimwengu huunganisha viumbe vyote kwa ajili ya umoja kamili na
Mungu.
Msikilizaji mpendwa, katika siku ya leo tulioombee Kanisa ili liwe
kielelezo cha: umoja, amani, upendo na mshikamano. Tuwaombee wote waliojiweka wakfu
katika Roho Mtakatifu wakatimize kazi yao ya wakfu kwa furaha na amani.
Ninakutakieni
Sherehe njema na mwendelezo mzuri wa maisha ya furaha. Ninakukumbusha kuwa leo Mama
Kanisa anahitimisha kipindi cha Pasaka. Tumsifu Yesu Kristo . Tafakari imeletwa
kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.