Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha huduma ya upendo kwa watu wa Mungu!
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 16 Mei 2013 mara baada ya Maadhimisho ya
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae kilichoko mjini Vatican
amekutana na kuzungumza na Kamati kuu ya Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa
Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis inayoendelea na mkutano wake wa mwaka
hapa mjini Vatican chini ya uongozi wa Kardinali Oscar Andres Rodriguez Maradiaga,
Rais wa Caritas Internationalis.
Baba Mtakatifu amewaambia wajumbe hao kwamba,
Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki ni kielelezo cha upendo wa Kanisa kwa wahitaji,
jambo ambalo linabubujika kutoka katika undani na asili ya Kanisa lenyewe. Baba Mtakatifu
alipata fursa pia ya kusikiliza ushuhuda kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuhusu
kazi na utume unaotekelezwa na Caritas Internationalis ambayo mwaka huu inatarajia
kuzindua kampeni dhidi ya baa la njaa duniani.
Baba Mtakatifu anasema kwamba,
Kanisa linaweza kuonesha ukuu wa Mungu si kwa kutenda miujiza, bali kwa kushirikishana
na kumegeana upendo ambao Mwenyezi Mungu amekwisha umimina katika mioyo ya waja wake.
Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa inakumbana na athari za myumbo
wa uchumi kimataifa ambao kimsingi unagusa nyanja mbali mbali za maisha ya mwanadamu:
kitamaduni na hata kiimani.
Mambo yote haya anasema Baba Mtakatifu yana madhara
makubwa katika maisha ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Caritas
inapaswa kutambua kwamba, inatumwa kuwajengea watu matumaini kwa kuwasaidia kuboresha
hali ya maisha ya wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kuna kinzani nyingi zinazojionesha
katika masuala ya fedha na uwekezaji kiasi cha kugumisha maisha ya mwanadamu na waathirika
ni watoto, wanawake na wazee.
Inasikitisha kuona kwamba, licha ya utajiri mkubwa
wa rasilimali ya dunia, lakini bado kuna watu wanateseka kutokana na: umaskini, magonjwa,
baa la njaa, wakati huo huo wengine wanatumia maendeleo ya sayansi kwa ajili ya kukumbatia
utamaduni wa kifo. Hizi ni dalili za kumong'onyoka kwa misingi ya maadili na utu wema.
Baba
Mtakatifu amegusia pia umuhimu wa Caritas kuwa ni chombo cha faraja kwa wahanga wa
vita na mamillioni ya wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kutoka katika maeneo yao
kwa kutafuta hifadhi ya maisha. Mama Kanisa anachangamotishwa kuwahudumia kwa moyo
wa upendo na mshikamano wa dhati: kwa kujitoa bila ya kujibakiza katika huduma ya
afya, elimu na maendeleo endelevu, kwa kutambua kwamba, Kanisa halina budi kuchukua
ile sura ya Msamaria mwema ambaye kimsingi ni Kristo mwenyewe ili kuwajengea watu
uwezo wa kujiletea maendeleo yao wenyewe!
Baba Mtakatifu anasema, watakatifu
mbali mbali ndani ya Kanisa walijitahidi kusoma alama za nyakati na kutafuta njia
ya kuweza kuyapatia ufumbuzi matatizo yaliyokuwa yanawasibu ndugu zao katika Kristo.
Huu ndio msingi wa tasaufi ya upendo inayomsukuma mwamini kujitosa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha
na utume wa Kanisa.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amegusia hali ya wakimbizi
kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee kutoka Syria ambako
hadi sasa inakadiriwa kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi millioni moja. Kuna wahamiaji
wanaoteseka na kudhulumiwa kwa kufanyishwa kazi za suluba kwa ujira kidogo. Haya ni
maeneo ambayo yapaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa katika huduma ya upendo.