Watanzania wanaoishi Roma kusali kwa ajili ya kuombea amani, umoja na mshikamano wa
kitaifa hapo Jumamosi, tarehe 18 Mei 2013
Watanzania wanaosoma na kuishi Roma, Jumamosi tarehe 18 Mei 2013 wataadhimisha Ibada
ya Misa takatifu kwa ajili ya kuombea amani, upendo na mshikamano miongoni mwa watanzania
wakati huu Tanzania inapopitia kipindi cha hali ya wasi wasi na majonzi makuu kutokana
na vurugu za kidini. Hii itakuwa ni fursa pia kwa watanzania kusherehekea umoja na
mshikamano wao wa kitaifa. Ibada hii itafanyika kwenye Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu
Petro, mjini Roma.
Taarifa iliyotolewa na viongozi wa wanafunzi watanzania
wanaosoma Roma inaonesha kwamba, watanzania watatumia nafasi hii pia kuwaaga wale
ambao wamehitimu masomo yao katika nafasi mbali mbali na sasa wako tayari kurudi Tanzania
kuendelea kujenga Kanisa na Nchi kwa ujumla. Itakumbukwa kwamba, hii pia ni nafasi
kwa ajili ya kuwapongeza watanzania waliopiga hatua mbali mbali katika maisha ya wito
wao kama Makleri na Watawa.