Katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka 1,700 ya Azimio la Milano, Baba Mtakatifu
Francisko ametuma ujumbe wa matashi mema kwa Kardinali Angelo Scola wa Jimbo kuu la
Milano, Kaskazini mwa Italia. Maadhimnisho haya yanapambwa na uwepo wa Patriaki Bartholomeo
wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli.
Baba Mtakatifu katika
ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican
anamtakia kheri na baraka, Yeye pamoja na wageni wote wanaoshiriki katika Maadhimisho
haya. Azimio hili, ulikuwa ni mwanzo wa uhuru wa kidini kwa Wakristo, ukiwa pia ni
mwanzo wa Injili ya Kristo kupenya katika maisha na hivyo kuwa ni chachu ya mwanzo
wa utamaduni wa wananchi wa Bara la Ulaya.
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu
Francisko anawaalika Wakristo kwa pamoja kutolea ushuhuda wao wakiongozwa na Roho
Mtakatifu, ili Ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu uweze kuenea Barani Ulaya na sehemu
nyingine za dunia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, uhuru wa kuabudu utaheshimiwa
na Serikali husika ili kutoa nafasi kwa waamini kushuhudia imani yao hadharani pamoja
na kuendelea kuchangia katika mchakato wa maisha ya mwanadamu kiroho na kimwili.
Baba
Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kuwahakikishia wajumbe wote kwamba, yuko pamoja
nao kwa njia ya sala na sadaka yake.
Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho haya
yaliyofanyika Jumatano tarehe 15 Mei 2013 yanaongozwa na kauli mbiu "tena mtaifahamu
kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru". Tukio hili limehudhuriwa pia na viongozi mbali
mbali wa Kanisa na Serikali kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Milano.