Fedha itumike kwa ajili ya huduma na wala si kutawala watu maskini!
Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza Mabalozi wapya waliowasilisha hati zao za utambulisho
mjini Vatican Alhamisi, tarehe 16 Mei 2013 na kusema kwamba, hali hii inaonesha utashi
wa kutaka kushirikiana na Vatican katika mchakato wa kumletea mwanadamu maendeleo
endelevu.
Baba Mtakatifu anasema, katika ulimwengu wa utandawazi kumekuwepo
na maendeleo makubwa katika sekta ya afya, elimu na njia za mawasiliano ya jamii,
lakini bado kuna mamillioni ya watu wanaoendelea kuishi katika umaskini wa hali na
kipato; hofu na wasi wasi, kiasi hata cha kukata tamaa hata katika nchi tajiri zaidi
duniani.
Furaha ya kuishi inaendelea kupungua siku hadi siku na matokeo yake
ni vitendo vya jinai vinazidi kuongezeka na umaskini kushamiri. Utu na heshima ya
mwanadamu vinaendelea kuathirika siku hadi siku, hii yote ni kutokana na mwanadamu
kupenda mno fedha kiasi cha kusahau utu na heshima ya binadamu. Hizi ndizo athari
zinazotokana na myumbo wa uchumi kimataifa. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga
na kudumisha moyo wa mshikamano unaosimikwa katika kanuni ya auni kwa ajili ya mafao
ya wengi pamoja na kuzingatia sheria na kanuni za fedha na uchumi.
Ubinafsi
umepelekea watu kushindwa kutekeleza wajibu wao katika Jamii kwa kutaka kujijengea
nguvu ya kiuchumi bila mipaka. Hiki ni kielelezo makini cha kutaka kumng'oa Mwenyezi
Mungu katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu na kuishi pasi ya kuzingatia kanuni
maadili ambayo kimsingi yameandikwa katika dhamiri ya mwanadamu. Ikumbukwe kwamba,
maadili yanajenga uhusiano wenye uwiano makini katika Jamii. Baba Mtakatifu anawaalika
viongozi wa Serikali na wachumi kusaidia mchakato wa kuboresha hali ya maisha ya watu
maskini badala ya kuwaibia na kuwatumbukiza katika maafa!
Jumuiya ya Kimataifa
haina budi kufanya mageuzi makubwa katika masuala ya fedha na uchumi yanayozingatia
kanuni maadili kwa ajili ya mafao ya wengi, jambo linalohitaji sera makini na ujasiri
kutoka kwa wanasiasa. Fedha itumike kwa ajili ya kutoa huduma na wala si kutawala
watu! Matajiri wakumbuke kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kuwasaidia maskini kuondokana
na hali yao ya umaskini, kwa kuwaheshimu na kuwathamini, hali ambayo inapaswa kujionesha
katika mshikamano wa kimataifa katika masuala ya fedha na uchumi.
Baba Mtakatifu
Francisko anabainisha kwamba, Kanisa kwa upande wake linaendeleza mchakato wa maendeleo
ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa ajili ya mafao ya wengi, changamoto kwa viongozi
wa kisiasa kujitoa kwa dhati kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wao, daima wakitafuta
mafao ya wengi, hali ambayo itajenga na kuimarisha amani na utulivu kati ya watu.
Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kuendelea kuchangia kwa hali na mali katika
maendeleo ya nchi zao, huku wakitolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake
inayojionesha kwa njia ya upendo na mshikamano wa kidugu! Hakuna sababu ya kuogopa
wala kukata tamaa. Baba Mtakatifu Francisko anawatakia kheri na baraka Mabalozi wapya
waliowasilisha hati zao za utambulisho mjini Vatican na kwamba, wataendelea kupata
ushirikiano wa dhati na viongozi wa Vatican wanapotekeleza wajibu na dhamana yao hapa
Vatican.