2013-05-15 09:51:58

Vatican kushiriki katika Onesho la 55 la Sanaa Kimataifa mjini Venice


Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema kwa mara ya kwanza kabisa katika historia, Vatican itashiriki kwenye Onesho la 55 la Sanaa Kimataifa litakazofanyika huko Venice, Venezia kuanzia tarehe Mosi, Juni hadi tarehe 24 Novemba 2013.

Lengo na ushiriki wa Vatican katika maonesho haya ni kujenga na kuimarisha utamaduni wa majadiliano katika medani mbali mbali za maisha. Hili ni tukio linaloshirikisha wadau mbali mbali katika sanaa na kwamba, maonesho haya si wakati wa kutafuta soko bali ni kudhihirisha uzuri wa sanaa kama kipaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu kinachopaswa kuendelezwa kwa mafao ya mtu binafsi na jamii inayomzunguka.

Katika onesho hili, Kardinali Ravasi anasema kwamba, Baraza la Kipapa la Utamaduni limeamua kuwasilisha Sura Kumi za Kitabu cha Mwanzo zinazoonesha kazi ya Uumbaji, jambo ambalo ni muhimu sana katika tamaduni na Mapokeo ya Kanisa. Sura hizi zinabainisha kwa namna ya pekee kazi ya uumbaji inayoonesha asili ya mwanadamu; ni sura zinazoonesha pale dhambi ilipoingia katika sura ya nchi na madhara yake katika maisha ya mwanadamu pamoja na mipango iliyofuatia mara baada ya mafuriko kutokea.

Kwa namna ya pekee, Kardinali Gianfranco Ravasi anabainisha kwamba, mada zinazowasilishwa kwenye Onesho hili zinajikita zaidi katika: Kazi ya Uumbaji, Madhara ya dhambi na Mtu Mpya. Baraza la Kipapa la Utamaduni limechagua picha maalum zitakazooneshwa huko Venice na amechukua fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru Wasanii waliojitoa kwa moyo mkuu kutekeleza wajibu na dhamana hii ambayo ni muhimu na inafumbata utajiri mkubwa wa majadiliano, amana na urithi mkubwa wa binadamu.

Akishiriki katika mkutano huu na waandishi wa habari, Professa Paolo Barata, Mkurugenzi mkuu wa "Venice Art Biennale" ameishukuru Vatican kwa utayari na moyo wa kuweza kushiriki katika maonesho haya kama jukwaa linalopania kukuza na kudumisha majadiliano yanayowahusisha wasanii kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Kwa njia hii washiriki wanapata fursa ya kukuza sanaa na utajiri wao kwa kulinganisha na mchango unaotolewa na wasanii wengine wanaoshiriki. Kuna hatari kwamba, kazi za sanaa zikageuzwa kuwa ni bidhaa zinazouzwa sokoni kiasi cha kupunguza nafasi na utajiri wake katika maisha ya Jamii husika. Huu utakuwa ni wakati kwa watazamaji na wasanii wenyewe kujenga pia utamaduni wa kufanya tafakari ya kina!

Kwa upande wake, Professa Antonio Paolucci anasema, Onesho hili la Kimataifa litakuwashirikisha wasaanii wengi kutoka sehemu mbali mbali za dunia; wote hawa wanakuja wakiwa na lugha na ufundi wao ambao utachambuliwa na kufanyiwa tathmini ya kina mintarafu kazi ya Uumbaji na uharibifu ambao umeendelezwa duniani kwa njia ya vita, uharibifu wa mazingira na ulaji wa kutupwa. Katika kinzani na misuguano, hapo cheche za maendeleo zinaibuliwa sanjari na mchakato wa kulinda na kutunza mazingira; kuzuia mmomonyoko wa ardhi pamoja na matumizi bora ya maliasili ya dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.