2013-05-15 07:43:06

Umuhimu wa utawala bora kama njia ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa


Baraza la Maaskofu Katoliki Mali kunako mwaka 2010 wakati wa Maadhimisho ya kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 ya uhuru wa bendera kutoka kwa Wafaransa waliandika Waraka wa kichungaji kwa waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Mali kwa kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 tangu walipojiapatia uhuru wa bendera sanjari na changamoto zilizokuwa mbele yao. RealAudioMP3

Maaskofu walibainisha kwamba, Serikali na wadau mbali mbali wa maendeleo ya mwanadamu kiroho na kimwili walikuwa na jukumu la kuibua mbinu mkakati wa maboresho ya hali ya maisha ya wananchi wa Mali, kwani wengi walikuwa wanaogelea katika dimbwi la ujinga, maradhi na umaskini wa hali na kipato; mambo ambayo ni hatari katika kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki lilikazia kwa namna ya pekee utawala bora ambao ulikuwa unapania kuongoza mchakato wa huduma ya upatanisho, haki na amani. Kanisa linatambua dhamana na wajibu wake unaolisukuma kushirikiana na wadau mbali mbali katika kutafuta mafao ya wengi. Jamii inapaswa kujengeka katika msingi unaoheshimu utawala wa sheria, kama alivyobainisha Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa Kichungaji, Africae Munus, Dhamana ya Afrika.

Chaguzi ziwe ni jukwaa la Jamii kuelezea maamuzi yao ya kisiasa na ni ishara ya uhalali kwa matumizi ya madaraka. Watu wajitahidi kuheshimu Katiba, chaguzi ziwe: huru zikizingatia haki na uwazi. Maaskofu wa Mali wanasema, Kanisa litaendelea kutoa ushirikiano wa dhati na Serikali pamoja na wapenda amani ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Kanisa linapenda kujielekeza zaidi katika mchakato unaopania maboresho katika sekta ya uchumi, siasa, jamii, maadili na utunzaji bora wa mazingira.

Maaskofu Katoliki wa Mali wanabainisha kwamba, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, inasikitisha kuona kwamba, ukabila, rushwa na ufisadi; baadhi ya watu kujisikia kuwa wako juu ya sheria pamoja na uvunjifu wa misingi ya haki na amani vimeongezeka maradufu nchini humo. Baadhi ya wanasiasa wamekuwa na uchu wa mali na madaraka; wameendelea kuonesha ubinafsi na matumizi mabaya ya madaraka, kiasi cha kukwamisha mchakato wa kuwaletea wananchi wa Mali maendeleo endelevu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Mali linabainisha kwamba; haki, amani na upatanisho wa kweli ni nyenzo muhimu sana ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo nchini humo. Maaskofu wanasema, upembuzi huu yakinifu wanaoutoa kwa kuzingatia dhamana na wajibu walio nao kwa ajili ya maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wananchi watambue na kuthamini haki na wajibu wao kama raia na kamwe wasiogope uadui au kukosa umaarufu kwa kuonesha msimamo katika maisha adili na manyofu. Kama waamini wanachota nguvu na ujasiri kutoka kwa Kristo mfufuka, ambaye kwa kifo chake ameushinda ulimwengu.










All the contents on this site are copyrighted ©.