Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kumwendea Yesu na analiongoza Kanisa katika Ukweli!
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea na Katekesi
kwa kuchambua Kanuni ya Imani, ambayo kimsingi ni muhtasari wa Imani ya Kanisa. Roho
Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Yesu anamwita Roho Mtakatifu
kuwa ni Roho wa Ukweli.
Baba Mtakatifu amechambua kazi za Roho Mtakatifu kwa
kusema kwamba, katika ulimwengu mamboleo watu wana mashaka kuhusu ukweli, lakini Kanisa
lina amini kwamba, ukweli upo na unapatikana kwa njia ya imani kwa Yesu Kristo, Neno
wa Mungu aliyefanyika mwili.
Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kumwendea
Yesu; anayeliongoza Kanisa katika utimilifu wa ukweli. Ni msaidizi aliyetumwa kutoka
kwa Yesu Mfufuka, ili kuwakumbusha yale yote aliyofundisha Yesu wakati akiwa bado
hapa duniani pamoja na kuwaimarisha waamini ili kuchuchumilia kweli za wokovu.
Baba
Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Roho Mtakatifu ni chemchemi ya maisha mapya katika
Kristo anayewawezesha waamini kuwa na "jicho la imani" linalowawezesha kujishikamanisha
na Neno la Mungu, pamoja na uelewa wa kina wa maana yake ili kuweza kuumwilisha katika
uhalisia wa maisha ya kila siku.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini
kujiuliza swali la msingi, ikiwa kama wako wazi kwa nguvu za Roho Mtakatifu kama alivyokuwa
Bikira Maria. Hata leo hii Fumbo la Utatu Mtakatifu linaendelea kukaa katika mioyo
ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza
katika ukweli pamoja na kuwasaidia kukuza urafiki na Kristo kila siku ya maisha kwa
njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa.
Baba
Mtakatifu anawatakia waamini wote heri na baraka katika Maadhimisho ya Siku kuu ya
Pentekoste. Ni matumaini yake kwamba: mapaji ya hekima, furaha na amani yatawaongoza
waamini pamoja na familia zao katika njia ya ufuasi makini wa Kristo. Anawataka waamini
kuendelea kuungana na Bikira Maria kusali kwa ajili ya faraja na nguvu ili kuimarisha
imani kwa Kristo na Kanisa lake. Anawataka wawe mashahidi wa Kristo katika hija ya
maisha yao hapa duniani. Kila mwamini ajitahidi kumfahamu Kristo na Ukweli huku wakidumu
katika Ukristo wao kwani Ukristo si jambo la mpito!
Kwa namna ya pekee, Baba
Mtakatifu Francisko alitambua uwepo wa waamini na mahujaji kutoka Jimbo la Arezzo-Cortona-San
Sepolcro, Chieti- Vasto, Pitigliano-Savona- Orbetello waliomiminika kwa wingi kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, wakisindikizwa na viongozi wao wa Kanisa.
Amewataka kuwa ni alama makini ya upendo wa Mungu na vyombo vya amani katika medani
mbali mbali za maisha.
Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, shule zinazomilikiwa
na kuendeshwa na Kanisa Katoliki zina nafasi ya pekee katika jamii na kwamba, dhamana
hii inapaswa kutekelezwa kwa kushirikiana na Familia sanjari na kutambua nafasi yake
katika Jamii husika.
Anawataka vijana kujitahidi kuuiga mfano wa Bikira Maria
ili waweze kuwa ni faraja kwa wale wanaomboleza na amani kwa wenye majonzi na wapweke.
Wagonjwa wametakiwa kupokea hali yao ya ugonjwa kwa imani, huku wakijiachilia mikononi
mwa Mwenyezi Mungu na wanandoa wapya wadumishe uaminifu wao kama kikolezo cha furaha
ya kweli.