2013-05-15 08:02:45

Miaka 150 tangu Wamissionari wa kwanza walipotua Zanzibar


Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inaendelea kukushirikisha Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2013, leo tunayaangalia matukio makuu ya kihistoria kwa upande wa Kanisa la Tanzania. Kutujuza zaidi ndani ya viunga vya Radio Vatican ni Sr. Gisela Upendo Msuya. RealAudioMP3
Tunapotafakari mwaliko huu wa kusimama imara katika imani, historia inatukumbusha pia kuwa miaka takribani 150 iliyopita, imani hii tunayoiishi na kuiadhimisha ilitufikia kupitia visiwa vya Zanzibar. Yesu Kristo, aliye Mlango wa Imani, ni Njia vilevile inayotuelekeza na kutuongoza kwenye Uzima. Yote huanzia na kuishia kwake. Hata hivyo, Yeye aliye Njia na Mlango hutufungulia “njia” nyingine nyingi na “milango” mingine mingi inayotuelekeza kwake Yeye aliye utimilifu wa yote.
Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu walipofika Zanzibar, mnamo mwaka 1860, hawakuishia hapo, bali wakitokea katika visiwa hivyo waliivusha mbegu ya imani hadi Tanganyika ya wakati huo na kuanza kuipanda katika mji wa Bagamoyo mnamo mwaka 1868. Mbegu hii ya imani iliendelea kuchipuka na kukua kupitia wamisionari wa mashirika mbali mbali; wakiwemo Wamisionari wa Afrika, Wabenediktini wa Mt. Ottilia na wengine wengi baada yao, ambao wote katika ujumla wao walikuja kwa lengo la kuinjilisha na kuhakikisha kuwa imani inaota mizizi yake katika maeneo ya nchi yetu.
Wamisionari hawa pamoja na kuwa na karama mbali mbali, waliunganishwa na lengo moja ambalo lilikuwa ni kutangaza habari njema. Kwa sababu hiyo, kila kundi, kwa wakati wake na kwa namna yake limetoa mchango wake uliotukuka, ama katika kupanda au katika kumwagilia mbegu na mche wa imani, na Mungu ameendelea kuukuza huu mche wa Imani (Rej. 1Kor 3:6).
Kumbukumbu hii inapaswa kuijaza mioyo yetu shukrani kwa Mungu aliyetupatia zawadi ya imani, zawadi iliyo kuu ya upendo wake. Shukrani yetu inapaswa, hata hivyo, kuvuka mipaka ya kubaki katika maneno tu na kuwa tendo la kudumu kiaminifu katika imani, kuifanya imani kuwa dira inayoongoza kila tendo la maisha yetu ya kila siku na kuhakikisha kuwa imani tuliyoipokea inazidi kustawi na kushamiri.
Mwaka wa Imani na Mkutano wa Kawaida wa Kumi na Tatu wa Sinodi ya Maaskofu
Mwezi Oktoba 2012, kuanzia tarehe 7 hadi 28, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alikutana Roma na Maaskofu kutoka ulimwenguni kote kwa ajili ya Sinodi ya 13 ya Kawaida ya Maaskofu iliyokuwa na mada: “Uinjlishaji Mpya kwa ajili ya Kueneza Imani ya Kikristo”. Sinodi hii ilikuwa na lengo la kuzindua programu ya Uinjlishaji Mpya. Sinodi ilitafakari kwa kina njia mpya na muafaka zitakazolisaidia Kanisa na wanakanisa wote kuifanya imani kuwa ni sehemu ya uhalisia wa maisha ya kila siku ya waamini, kwa kuiishi kwa ari inayokuwa na kukomaa katika maneno, matendo na mienendo ya maisha.
Tarehe 11 Oktoba 2012, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alizindua Mwaka wa Imani ambao utafikia kilele chake wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme tarehe 24 Novemba 2013. Lengo msingi la Mwaka wa Imani limewekwa bayana na Baba Mtakatifu katika hati yake Porta Fidei (Mlango wa Imani).
Mwaka wa Imani ni mwaliko wa kurudia upya ungamo la imani na kulitia katika matendo ya maisha ya kila siku. Ni wakati wa kupokea kwa shukrani zawadi ya imani ambayo kwa ubatizo mlango wa mahusiano ya kina na Mungu unafunguliwa. “‘Mlango wa Imani’ (Mdo 14:27) daima umefunguliwa kwa ajili yetu na kutuongoza katika muungano na Mungu na kutuingiza ndani ya Kanisa lake.
Inawezekana kuvuka kizingiti hicho pale neno la Mungu linapotangazwa na moyo unapojiruhusu kuundwa kwa kugeuzwa na neema. Kupita katika mlango huo ni kuanza safari itakayodumu kwa maisha yote.” Safari hii kwa wakati wa sasa inabeba pia mwaliko wa Uinjilishaji Mpya kwa sababu zipo dalili na maelekeo makubwa ya Wakristo kusahau au/na kuzembea maisha ya imani.

Imani ya Kanisa sio tu matamko mbalimbali ya Kanisa, bali ni uhusiano hai na Yesu Kristo, aliye Kichwa cha Kanisa, na uhusiano na Mwili wake, yaani Kanisa. Tunachokiamini ni Ukweli uliofunuliwa kwetu na Yule ambaye ndani yake tunaamini, Yesu Kristo, Ukweli unaoendelezwa na Kanisa chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Kwa hivi, Kanisa lina wajibu huo wa kuiendeleza imani kwa kuwa, “Kazi ya kueneza Injili ni wajibu na ndio utume halisi wa Kanisa.”Njia ya kutekeleza wajibu huo ni “kutweka mpaka kilindini”, ambako ndiko dhamana ya wakati huu wa kihistoria kwa Kanisa iliko. Hatua hii ya matumaini italiwezesha Kanisa kuchukua hatua mpya mbele katika historia.








All the contents on this site are copyrighted ©.