2013-05-14 08:05:32

Waamini wanaalikwa kujiunga na Papa Francisko kuufunga Mwezi wa Bikira Maria, hapo tarehe 31 Mei 2013 kwa Rozari Takatifu


Kardinali Angelo Comastri, Makamu Askofu wa Mji wa Vatican anawakaribisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 31 Mei 2013, kuanzia saa 2:00 Usiku kwa ajili ya kusali Rozari Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama kielelezo cha kufunga Mwezi wa Bikira Maria.

Itakuwa ni fursa kwa waamini kusali pamoja na kusikiliza tafakari itakayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko siku hiyo! Hii ni siku maalum kwani Kanisa pia litakuwa linafanya kumbu kumbu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeth, kielelezo makini cha upendo kwa Mungu na jirani.

Kwa wakazi wa Roma na viunga vyake wanaambiwa kwamba, hakuna haja ya kutafuta tiketi ya kuingilia, tiketi ni utashi na miguu yako! Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwepo na idadi kubwa ya waamini wanaoshiriki katika Katekesi, Ibada na Sala ya Mchana inayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kila Jumapili. Huu pengine ni mwanzo wa matumaini mapya.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alipokuwa anasali Rozari Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu mjini Roma, alisema kwamba, Bikira Maria anawafundisha waamini kuwa na uhuru wa kweli na kuanza hija ya ukomavu katika imani wakiwa na maamuzi makubwa, daima wakiwa na ujasiri bila kuyumbishwa.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili aliwahi kusema, kati ya sala zinazogusa moyo wake ni Rozari Takatifu ambayo ni muhtasari wa Injili, yaani maisha na utume wa Yesu. Mwamini anaposali na kutafakari matendo makuu ya Mungu kwa njia ya Rozari Takatifu anakumbatia maisha ya mtu binafsi, familia, taifa na dunia katika ujumla wake. Rozari Takatifu ni sala ya kawaida inayodhihirisha hija ya maisha ya mwanadamu.

Mama Theresa wa Calcutta aliwahi kukumbushia kwamba, anaposali Rozari Takatifu, Yesu anamkirimia fadhila ya upendo moyoni mwake, kiasi kwamba, anajisikia wajibu wa kutoka nje na kwenda kuwamegea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha. Mwenyeheri Mama Theresa wa Calcutta anawahimiza waamini kusali Rozari takatifu kwa hakika wataweza kuonja siri ya mafanikio katika maisha ya kiimani.







All the contents on this site are copyrighted ©.