2013-05-14 07:12:15

Uhuru wa kidini unaendelea kupungua sehemu mbali mbali za dunia!


Tume ya Serikali ya Marekani inayoangalia masuala ya kimataifa kuhusu uhuru wa kidini katika taarifa yake ya mwaka 2013 inaonesha kwamba, uhuru wa kidini unaendelea kupungua sehemu mbali mbali za dunia, jambo ambalo linachangiwa kwa namna ya pekee na waamini wenye misimamo mikali ya kidini na baadhi ya serikali kutotekeleza wajibu wake barabara. RealAudioMP3

Taarifa hii kwa upande wa Bara la Afrika inaonesha kwamba, Eritrea na Sudan ni kati ya nchi ambazo zina hali mbaya zaidi zikifuatiwa na: Misri na Nigeria. Kuna baadhi ya Serikali ambazo zimeendelea kuwa ni kikwazo cha uhuru wa kuabudu na ufundishaji wa dini shuleni, hali ambayo wakati mwingine inagusa uhuru wa dhamiri ya mtu.

Eritrea na Misri ni nchi ambazo kuna uvunjifu mkubwa wa uhuru wa kidini, watu kuwekwa kizuini kwa muda mrefu pamoja na madhulumu yanayofanywa kwa misingi ya kidini. Hali inaendelea kutisha nchini Nigeria kadiri ya taaira hii kwani kuna madhulumu makubwa ya kidini yanayofanywa dhidi ya Wakristo nchini Nigeria.
Taarifa hii inabainisha kwamba, tangu mwaka 1999 kuna watu zaidi ya 14, 000 ambao wamepoteza maisha kutokana na mashambulizi na madhulumu ya kidini kati ya Wakristo na Waislam nchini Nigeria.

Mabadiliko ya Katiba nchini Misri, Somalia, Libya na Sudan yanaendelea kufanyika hali ambayo wakati mwingine imeibua kinzani na migogoro ya kidini. Muswada wa Katiba ni jambo muhimu sana hata ikiwa kama Katiba yenyewe itashindwa kutekelezwa barabara, kwani kimsingi hii inapaswa kuwa ni Sheria Mama.

Katika nchi ambazo Tume hii imefanya utafiti na uchunguzi wake, imebainisha kwamba, kuna nchi 23 ambazo dini ya Kiislam inatambulika kuwa ni dini ya Serikali mintarafu Katiba ya Nchi. Nchi nyingine 33 katika Katiba zao, zinatamka wazi wazi kwamba, Serikali haina dini, lakini watu wake wana dini na imani zao zinazopaswa kuheshimiwa na kulindwa kikatiba.

Pamoja na ukweli huu, bado kuna vurugu na mashambulizi ya kidini yanayofanywa na watu binafsi, makundi ya watu, wapinzani wa serikali pamoja na vikundi vya kigaidi.

Tume inasema kwamba, Serikali husika na vyombo vya ulinzi na usalama katika baadhi ya nchi vimeshindwa kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu hata kama umebainishwa na Katiba zao, jambo ambalo linasababisha baadhi ya wananchi kukosa imani na serikali zao! Sheria na haki sawa kwa raia ni mambo yanayopaswa kutekelezwa kwa makini bila ubaguzi ili kujenga na kudumisha misingi ya uhuru wa kuabudu, changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa katika nyakati hizi.








All the contents on this site are copyrighted ©.