2013-05-14 10:57:40

Mwombeni Roho Mtakatifu awakirimie moyo wa kupenda kwa unyenyekevu!


Waamini wanapaswa kuwa na moyo mkuu wenye uwezo wa kupenda, kinyume kabisa na ubinafsi uliojionesha katika maisha ya Yuda Iskarioti, aliyejikuta mpweke kiasi hata cha kumsaliti Bwana wake.

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae kilichoko mjini Vatican, Jumanne, Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya Mtume Mathias inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Mei.

Wafuasi wa Kristo wanapaswa kutambua kwamba, maisha yao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanayopaswa kuishirikisha kwa jirani zao na kwa jinsi hii wataweza kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo. Yesu alionesha upendo wa hali ya juu kabisa kwa kuyatoa maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa dunia, kinyume chake, Yuda Iskarioti alikata tamaa na hatimaye, kuitema zawadi ya maisha.

Umaskini unapaswa kufahamika katika huduma kwa wahitaji na wala si katika masuala ya kisiasa na hali ya kujisikia kama alivyoonesha Yuda Iskarioti wakati Maria Madgalena alipokuwa anampaka Yesu mafuta yenye marashi. Anayependa yuko tayari kuyamimina maisha yake kwa ajili ya jirani zake na kamwe hawezi kutawaliwa na ubinafsi.

Dhamana hii inatekelezwa katika Familia na Jamii ya watu wanaomzunguka. Mtu anayetawaliwa na ubinafsi na dhamiri iliyokufa kiasi cha kujishikamanisha mno na fedha, matokeo yake ni kuangamia kama ilivyokuwa kwa Yuda Iskarioti.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wakati huu wa Novena ya Roho Mtakatifu, kumwomba Roho Mtakatifu ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia moyo mkuu wenye uwezo wa kupenda kwa unyenyekevu na kuwaondoa kwenye njia ubinafsi ambayo itawapoteza milele.







All the contents on this site are copyrighted ©.