2013-05-14 09:30:19

Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa yaanza mkutano wake wa mwaka hapa Roma


Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kutoka katika nchi 150 wanaendelea na mkutano wao wa mwaka uliofunguliwa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na unatarajiwa kufungwa rasmi hapo tarehe 18 Mei 2013.

Katika hotuba yake ya ufunguzi siku ya Jumatatu tarehe 13 Mei 2013, Kardinali Filoni amesema kwamba, Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa yanatekeleza dhamana na wajibu wake katika mazingira hatarishi; sehemu ambako kuna madhulumu na nyanyaso za kidini; umaskini wa hali na kipato; kinzani za kivita na kijamii pamoja na umati mkubwa watu kuendelea kusukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hali zote hizi zinachangia kwa namna ya pekee katika kuibua na kutekeleza mikakati inayopangwa na Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa.

Kardinali Filoni anawataka wajumbe kuibua kanuni na mikakati itakayotekelezwa kwa kutambua kwamba, wao wanatumwa kutoa huduma katika nchi zao, wakisukumwa na imani. Kuna haja kwa wajumbe kufanya marekebisho katika mbinu za Uinjilishaji kwa kusoma alama za nyakati zitakazoliwezesha Kanisa kumfikishia mwanadamu wa leo ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuzima kiu ya udadisi wa maisha yake kwa kujikita katika mshikamano wa udugu.

Mashirika haya yanatekeleza dhamana hii nyeti ndani ya Jamii kwa kuongozwa na msingi wa imani na kwamba, huu ni utume wa Kanisa kwa ajili ya binadamu wa nyakati hizi.







All the contents on this site are copyrighted ©.