2013-05-14 07:40:16

Familia ni kiota cha maisha ya mwanadamu na mahali pa kwanza anapoonjeshwa upendo!


Sr. Maria Eugenia Thomas, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, familia ni kiota cha maisha ya binadamu, mahali pa kwanza kabisa ambapo mwanadamu anaonja upendo. RealAudioMP3

Ni mahali pa makuzi na malezi ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Familia inapaswa kukuza na kudumisha misingi ya upendo na mahusiano ya kina, sanjari na kufahamu wajibu wake unaopaswa kutekelezwa kwa moyo mkuu.

Sr. Eugenia anasema kwamba, utambulisho wa mtu katika Jamii unapata chimbuko lake katika maisha ya kifamilia na Jamii inayomzunguka mtu mwenyewe. Ndiyo maana kauli ya Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa kwa mwaka 2013 inakazia umuhimu wa kuimarisha na kuendeleza ushirikiano na mshikamano wa familia na makundi mbali mbali ya kijamii.

Kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu ndani ya Jamii, kuna haja kwa wazazi na walezi kuwa karibu zaidi na watoto wao ili kuwasaidia katika makuzi pamoja na kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku kwa amani na utulivu wa ndani.

Sr. Eugenia anakazia kwamba, dhamana ya malezi ya kiutu na kiimani ni nyeti sana katika maisha ya kifamilia, jambo ambalo wanafamilia wanapaswa kulitambua ili kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika mipango yao ya maisha. Familia ni Katekisimu ya kwanza ya: maisha ya imani inayoungamwa; inayoadhimishwa; inayomwilishwa katika maisha adili na yale ya sala. Ndiyo maana viongozi wa Kanisa wanasema, Familia inayosali kwa pamoja hiyo itashikamana na kudumu, changamoto kwa familia za Kikristo kuwa ni shule ya sala, haki, amani na utakatifu wa maisha.

Sr. Eugenia anasema, Roho Mtakatifu ataweza kuleta mabadiliko na kuumba upya sura ya nchi ikiwa kama atapewa nafasi kuanzia kwenye maisha ya kifamilia, kwani familia ni msingi wa maisha ya mwanadamu na chemchemi ya imani kwa Kristo na Kanisa lake. Ni mwaliko kwa wadau mbali mbali kuzisaidia familia kutekeleza wajibu wake kwa Kanisa na Jamii, kwa kutambua kwamba, familia zinashiriki pia katika kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu anaishiriki kwa utashi na mapenzi ya Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.