2013-05-13 07:35:57

Simameni kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili iliyopita, tarehe 12 Mei 2013, ambayo kwa Makanisa mengi duniani yaliadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana mbinguni sanjari na Siku ya 47 ya Upashanaji habari Ulimwenguni, aliungana na maelfu ya waamini waliokuwa wamemiminika mjini Vatican kusali pamoja Sala ya Malkia wa Mbingu.

Kwa namna ya pekee, ametoa salam na matashi mema kwa wananchi wa Italia, Mexico na Colombia ambao wamebahatika kupata watakatifu wapya aliowatangaza wakati wa Ibada ya Misa Takatifu. Amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, mashahidi wa Otranto aliowatangaza Jumapili iliyopita wawasaidie wananchi wa Italia kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi, huku wakijitahidi kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kwani kwa hakika Mwenyezi Mungu hawezi kuwaacha waja wake wanaomkimbilia kwa imani na matumaini thabiti hasa katika nyakati za shida na mahangaiko ya ndani.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali, ili kwa maombezi ya Mama Laura Montoya, Mwenyezi Mungu aweze kuleta ari na mwamko mpya zaidi wa utume wa Kimissionari na Uinjilishaji Mpya ndani ya Kanisa, lakini kwa namna ya pekee nchini Colombia. Kwa kufuata mfano wa Mtakatifu huyu, wananchi wa Colombia waweze kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa, daima wakiendelea kujitaabisha kwa ajili ya ujenzi wa amani, haki na maendeleo endelevu ya nchi yao.

Baba Mtakatifu Francisko amewaweka maskini, wagonjwa na wale wote wanaowahudumia chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Guadalupe Garcia Zavala. Anawaomba waamini na wananchi wa Colombia katika ujumla wao kuondokana na vitendo vya uhalifu na ukosefu wa amani na utulivu, daima wakijitahidi kutembea katika hija ya mshikamano wa kidugu.

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Mwenyeheri Padre Luigi Novarese, mwanzilishi wa vituo vya watu wa kujitolea kwa wagonjwa na wahudumu wa Msalaba katika hali ya ukimya, aliyetangazwa Jumamosi tarehe 11 Mei 2013, kwenye Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, Ibada iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma.

Padre Luigi Novarese katika maisha na utume wake, alileta mwamko wa pekee kabisa katika huduma za kichungaji kwa wagonjwa, kiasi cha kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa kundi kubwa la waandamanaji waliofika na kushiriki kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican mara baada ya maandamano kwa ajili ya kutetea Injili ya Maisha.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Baba Mtakatifu anaunga mkono juhudi zinazoendelea kufanywa na Kanisa Barani Ulaya kwa ajili ya kukusanya sahihi ili kulinda na kutetea kisheria viini tete ili visiwe ni vichokoo vya majaribio ya kisayansi.

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wale wote wanaojitoa kimasomaso kwa ajili ya kutetea utakatifu wa maisha ya mwanadamu. Amekumbusha kwamba, tarehe 15 hadi tarehe 16 Juni 2013 kutafanyika Maadhimisho ya Siku ya Injili ya Uhai, kama sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, hapa mjini Vatican.

Mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Baba Mtakatifu alisalimiana na viongozi wa Kanisa na wawakilishi mbali mbali waliohudhuria katika Ibada ya Misa Takatifu. Alitumia fursa hii pia kuzunguka na kusalimiana na waamini, mahujaji pamoja na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliokuwa wameupamba Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro.








All the contents on this site are copyrighted ©.