2013-05-13 07:56:06

Siku ya Mama Duniani! Jamani eti ni nani kama Mama?


Jumapili iliyopita, tarehe 12 Mei 2013 Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha Siku ya Mama Duniani, inayoonesha dhamana na wajibu wa akina mama katika maisha ya familia na jamii katika ujumla wake. Wanawake wamekirimiwa dhamana ya kutunza zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, na kuendelea kumtunza na kumlea hatua kwa hatua hadi pale anapojitegemea mwenyewe.

Hawa ni mama wa wale walio hai, kama ambavyo anasema Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili katika Waraka wake wa kichungaji “Mulieris Dignitatem”, Utu wa Mwanamke. Wanawake wanashiriki katika fumbo la uumbaji ambalo wamekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kutokana na umama wao. Kutokana na ukweli huu, watu wa ndoa wanamepewa dhamana ya nguvu ya uumbaji!

Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili anasema, kwa kawaida mwanamke amekirimiwa uwezo wa kuwa ni mama: kwa kutunga mimba, kulea na hatimaye wakati unapowadia kujifungua mtoto ambaye kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Jamii inapaswa kuwa na uelewa mpana na wenye tija kuhusu umama wa mwanamke usiogubikwa na sera tenge au utamaduni wa kifo unaopigiwa debe na baadhi ya watu kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Umama wa wanawake unajidhihirisha vyema katika maneno ya Bikira Maria na “nitendewe kama Bwana alivyonena” Hiki ni kielelezo kinachomwonesha mwanamke ambaye yuko tayari kabisa kubeba na kutunza zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Uzazi anasema Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili ni dhamana shirikishi kati ya mwanamke na mwanaume, ambao kwa pamoja wanayo haki ya kusema “huyu ni mtoto wetu”. Lakini hapa ieleweke kwamba, mwanamke anao wajibu mkubwa zaidi katika malezi na makuzi ya mtoto tangu pale anapokuwa bado tumboni mwa mama yake. Mtoto katika kipindi cha miezi tisa anamtegemea mama yake mzazi! Wanaume wanapaswa kutambua hili na kujitahidi kulienzi.

Hapa hakuna sera za haki sawa kwani mwanamke amekirimiwa kwa namna ya pekee kushiriki katika fumbo la maisha ya mwanadamu. Katika maisha yake, anaonja mchakato wa maisha ya mwanadamu hatua kwa hatua. Licha ya mchango mkubwa unaotolewa na mwanamke katika fumbo la maisha ya mwanadamu, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, anawaalika wanaume kushiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto wao, kwani wote kwa pamoja wanahitajika ili kujenga msingi wa ukomavu wa maisha ya mtu.








All the contents on this site are copyrighted ©.