2013-05-13 08:21:24

Ndoa za mseto na changamoto zake katika hija ya imani na malezi ya watoto!


Askofu mkuu Jean Laffitte, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Familia, hivi karibuni alijadili kuhusu ndoa za mseto kati ya Wakatoliki na Waamini wa dini nyingine na kati ya Wakatoliki na Waamini wa Madhehebu mbali mbali ya Kikristo kwa kusema kwamba, ni jambo ambalo linahitaji uangalifu mkubwa katika mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya mafao ya familia husika. RealAudioMP3

Hili ni jambo ambalo limekuwepo kwa miaka mingi Barani Afrika na Asia, lakini mwelekeo huu unakuja kwa kasi kubwa hata Barani Ulaya; matokeo ya ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ni mwelekeo wenye hatari na fursa nyingi katika maisha ya kiroho miongoni mwa wanafamilia. Ndoa ya mseto inaweza kuwa ni kati ya Wakatoliki na Waamini wa Makanisa mengine ya Kikristo kama vile Waluteri, Waanglikani au Makanisa ya Kipentekosti. Yote haya yanaonesha kwamba, upendo wa dhati unavuka mipaka ya imani, tamaduni na mahali anapotoka mtu. Lakini madhara yake ni makubwa pale ambapo wanandoa watashindwa kuheshimiana katika misingi ya imani yao, jambo ambalo linaweza kuwa ni kikwazo katika ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Ndoa Takatifu kadiri ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa Katoliki ni sehemu ya Fumbo la Kanisa, linaloonesha ule upendo wa dhati kati ya Yesu Kristo na Kanisa ambalo ni mchumba wake mwaminifu. Kwa Wakatoliki, Ndoa Takatifu ni Sakramenti ambayo kimsingi ni alama wazi ya muungano kati ya Kristo na Kanisa lake. Huu ni muungano wa daima hadi pale kifo kitakapowatenganisha. Kuna baadhi ya dini zinahalalisha ndoa za wake wengi pamoja na talaka.

Ili mwamini aweze kufunga ndoa ya mseto hana budi kwanza kabisa kupata kibali kutoka kwa Askofu wake mahalia, kwa misingi kwamba, watoto watakaozaliwa watabatizwa na kulelewa katika imani ya Kanisa Katoliki, jambo ambalo kwa haraka haraka linaweza kuonekana kuwa ni jepesi, lakini uzoefu na mang’amuzi ya kichungaji yanabainisha kwamba, kumekuwepo na ugumu kwa kiasi kikubwa, hasa katika nchi za Mashariki ya Kati na Asia.

Askofu mkuu Jean Laffitte anasema kwamba, haya ni mambo msingi yanaopasa kuangaliwa kabla mtu hajaanza mchakato wa kutaka kufunga ndoa ya mseto. Wanandoa watarajiwa watambue imani ya wenzi wao, dhamana na mchango wao katika kukuza na kuimarisha imani endapo watabahatika kufunga ndoa. Ni vyema wakajadiliana kuhusu malezi ya kiimani na kimaadili ya watoto wao kwa siku za usoni kadiri ya sheria za Kanisa, ili kuwawezesha waamini hawa kudumisha misingi ya imani na Mapokeo ya Kanisa.

Kwa waamini wanaotaka kuolewa katika misingi ya dini ya Kiislam wanapaswa kutambua kwamba, watoto watalelewa katika misingi ya dini ya Kiislam, kwani watalazimika kufuata dini ya baba yao mzazi. Katika nchi ambazo wamafuata Sharia ya dini ya Kiislam, ndoa kati ya Muislam na Mkristo imepigwa rufuku. Kuna tamaduni ambazo mwanamke hana sauti kumbe, hawezi kupewa dhamana ya kulea watoto wake katika misingi ya imani yake.

Askofu mkuu Jean Laffitte anakiri kwamba, katika nchi ambazo Waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo wameishi kwa amani na utulivu kwa miaka mingi, kama vile Lebanon, kuna maelewano mazuri kati ya wanandoa. Kumbe, kuna haja kwa waamini kuwa makini katika masuala ya ndoa na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na malezi ya watoto ambao kimsingi ni zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ukitaka kujitajirisha zaidi na uchambuzi wa kina kuhusu masuala ya kifamilia, unaweza kutembelea katika tovuti ya Baraza la Kipapa la Familia kwa anuani ifuatayo:
www.family.va








All the contents on this site are copyrighted ©.