Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani: Papa kutinga Brazil ili kuungana na vijana!
Yaani...!
Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 28 Julai
2013, atafanya hija ya kichungaji Rio de Janeiro, Brazil ili kushiriki katika Maadhimisho
ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Basi enendeni, mkawafanye
mataifa yote kuwa wanafunzi” Mt. 28:19.
Miezi minne
tangu alipochaguliwa kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko
anarudi tena Amerika ya Kusini, kwa kutembelea Brazil ambayo ina idadi kubwa ya Wakatoliki
duniani. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwasili mjini Rio de Janeiro jioni ya Jumatatu,
tarehe 22 Julai 2013 na kupokelewa na Mwenyeji wake kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Antonio Carlos Jobim wa Rio de Janeiro, na atabaki nchini humo kwa muda wa siku
saba. Jioni Baba Mtakatifu atamtembelea Rais wa Brazil Dilma Rousseff.
Jumanne,
tarehe 23 Julai 2013 baada ya safari ndefu, atapata mapumziko mafupi kwenye makazi
ya Sumarè, mjini Rio de Janeiro.
Jumatano, tarehe 24 Julai 2013 itakuwa ni
siku maalum kabisa ambayo Baba Mtakatifu Francisko ataitumia kwa ajili ya kufanya
hija ya maisha ya kiroho kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili wa Aparecida. Hapa
ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu.
Baadaye mchana, Baba Mtakatifu Francisko
na msafara wake watapata chakula cha mchana pamoja na Maaskofu na Waseminari kwenye
Seminari ya Yesu mchungaji mwema ya Aparecida. Baba Mtakatifu jioni, atatembelea na
kufungua Hospitali ya Mtakatifu Francisko inayotoa huduma kwa wagonjwa wa afya ya
akili.
Alhamisi, tarehe 25 Julai 2013, Baba Mtakatifu ataanza siku kwa kuadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwenye makazi yake ya muda hapo Sumarè mjini Rio de Janeiro.
Asubuhi atakaribishwa na kupewa ufunguo wa mji wa Rio de Janeiro pamoja na kubariki
bendera za Olympic.
Atatembelea Jumuiya ya Varginha na baadaye jioni, hapo
shughuli ya kuwakaribisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, itaanza kucharuka,
kiashilio cha Ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Shughuli
hii itafanyika kwenye ufukwe maarufu wa Copacabana ulioko mjini Rio de Janeiro.
Ijumaa,
tarehe 26 Julai 2013, Baba Mtakatifu ataianza siku hii kwa Ibada ya Misa Takatifu
na baadaye atashiriki katika kuwaungamisha baadhi ya vijana watakaoshiriki katika
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Tukio hili linafanyika kwenye Uwanja wa Quinta
da Boa. Atasalimiana na baadhi ya vijana wanaotumikia adhabu yao gerezani na mchana
atasali na vijana Sala ya Malaika wa Bwana. Mchana atapata fursa ya kukutana na kuzungumza
na Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Vijana na Wafadhili.
Siku hii itapambwa
kwa vijana kupata chakula cha mchana na Baba Mtakatifu Francisko. Jioni vijana watashiriki
pamoja na Baba Mtakatifu kuadhimisha Njia ya Msalaba kwenye ufuko wa Copacabana.
Jumamosi,
tarehe 27 Julai 2013 majira ya asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada
ya Misa takatifu pamoja na Maaskofu watakaokuwa wanahudhuria Siku ya 28 ya Vijana
Duniani pamoja na Mapadre, Watawa na Majandokasisi, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Sebastian. Baadaye atakutana na kuzungumza na wa viongozi wa Serikali, Kisiasa na
Kijamii nchini Brazil.
Maaskofu wa Brazil na msafara wa Baba Mtakatifu kwa
pamoja watapata chakula cha mchana kwenye Kituo cha Elimu cha Sumarè mjini Rio de
Janeiro. Jioni Baba Mtakatifu atashiriki katika mkesha wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana
Duniani katika Uwanja wa Campus Fidei.
Jumapili tarehe 28 Julai 2013, kitakuwa
ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Ibada ya Misa Takatifu na
baadaye atasali Sala ya Malaika wa Bwana. Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana
na msafara wake na jioni atakutana na kuzungumza na Kamati ya Uratibu ya Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini.
Baba Mtakatifu atakutana pia na
vijana wa kujitolea kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani na baadaye ataelekea
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Galeào/ Antonio Carlos Jobim wa Rio de Janeiro, tayari
kuagana na vijana pamoja na wenyeji wake. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko atakavyokuwa
anakunja jamvi la Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.
Anatarajiwa
kuwasili mjini Roma kwenye Uwanja wa Ciampino majira ya mchana. Kama kawa, Idhaa ya
Kiswahili Radio Vatican itahakikisha kwamba, “inakula nawe sahani moja” ili kukujuza
yale yatakayokuwa yanajiri katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa
Mwaka 2013.
Itakumbukwa kwama, Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili katika utume
wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alibahatika kutembelea Brazil mara nne; yaani
kunako mwaka 1980, 1982, 1991, 1997. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, kunako
mwaka 2007 alitembelea mji wa San Paulo na Aparecida, makao makuu ya Mkutano wa tano
wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini ambao pia Kardinali
Jorge Mario Bergoglio alishiriki pia.