Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani kumsimika Askofu mteule
Dr. Jacob E. Chimeledya mjini Dodoma
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Sherehe za kumsimika
Askofu Mteule Dk. Jacob Erasto Chimeledya (56), wa Kanisa Anglikani, Dayosisi ya Dodoma
zitakazofanyika Jumapili Ijayo kwenye Kanisa Kuu Dodoma itakayowahusisha viongozi
wa ndani na nje.
Hayo yamesemwa katika Ibada ya Jumapili, Mei 12, 2013 na Katibu
Mkuu wa Kanisa hilo Dicksoni Chilongani na kuthibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Dr. Rehema Nchimbi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani
Dodoma.
Akizungumza katika Ibada hiyo, Chilongani alisema, ili kuhakikisha
yaliyojitokeza Arusha hayatokei Dodoma, hatua zote za ulinzi na usalama zimechukuliwa,
na hivyo Kanisa limekubaliana na vyombo vya Usalama waumini watakaoingia Kanisani
hapo wakaguliwe (Screened) na vyombo maalum.
“Kutokana na kuwa na ugeni wa
Askofu Mkuu Justin Welby (57) ambaye ametawazwa rasmi kuwa Askofu Mkuu wa Cantebury
Machi 2013 atamsimika Askofu Dk. Chimeledya, tahadhari zote zimechuliwa, hivyo msibebe
mabegi makubwa maana mtapekuliwa na vyombo maalum”.alisema.
Akizindua Kanda
ya Kwaya ya Uvuke na Kununua Kanda Moja kwa Sh. Laki Moja, Dk. Nchimbi alisema, pamoja
na usalama kutoka kwa Mwenyezi Mungu waamini wanatakiwa kuwa na tahadhari hivyo amewaruhusu
waamini hao kumpigia simu iwapo wataona chochote kisicho cha kawaida popote walipo.
Hata
hivyo aliwataka wenye nyumba za wageni kuhakiki wateja wao na kuwatambua kwa taratibu
na sheria za kazi yao, na akawageukia wazee wa Kanisa hilo kuonesha jinsi walivyo
na wajibu wa kuwa Walinzi wa Kanisa la Mungu katika maeneo yao ya mitaa na kanisani.
Aidha
Katika Uzinduzi huo, Dk. Nchimbi alisema, Kanda hizo zinakwenda Sokoni ili kuponya,
kuokoa, kujenga Ndoa, kufundisha, na kuirejesha Jamii kufurahia Maisha Bora yaliyoko
mikononi mwa mwa Mungu, ambayo Jamii itayaoata tu ikiwa na Uadilifu na Uchaji mbele
za Mungu.