“Mitandao ya Kijamii: milango ya ukweli na imani; nafasi mpya za Uinjilishaji”.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari yameanzisha “Jukwaa” na uwanja ambao
watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanashirikishana mawazo, habari na maoni;
hapa ni mahali ambapo watu wanajenga mahusiano mapya sanjari na uundaji wa Jumuiya
mpya. Hivyo ndivyo Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, anavyoandika kwenye ujumbe wa Siku ya
47 ya Mawasiliano Duniani kwa mwaka 2013 inayoadhimishwa tarehe 12 Mei 2013 kwa kuongozwa
na kauli mbiu “Mitandao ya Kijamii: milango ya ukweli na imani; nafasi mpya za Uinjilishaji”. Baba
Mtakatifu anasema, ikiwa kama njia hizi zitatumika kwa busara na uwiano mzuri zinaweza
kuhamasisha majadiliano ambayo yakiendeshwa kwa heshima, kwa kuzingatia utu wa mtu;
uwajibaki na ukweli zinaweza kuchangia mchakato wa ujenzi wa amani kati ya watu na
hivyo kudumisha utulivu katika Familia ya Binadamu. Ubadilishanaji wa habari unaweza
kwa hakika kuwa kweli ni mawasiliano yanayolenga kujenga urafiki pamoja na kurahisisha
muungano kati ya watu. Ikiwa kama Mitandao ya kijamii inapewa changamoto hii kubwa
katika Jamii ya binadamu, wadau wakuu wanapaswa kujibidisha kuhakikisha kwamba, wanakuwa
wakweli kwa kutambua kwamba, nafasi hizi zinatumiwa si tu kwa ajili kushirikishana
mawazo na habari bali pia wahusika wenyewe. Maendeleo ya mitandao ya Kijamii yanahitaji
majitoleo: hapa watu wanajenga mahusiano na urafiki; wanatafuta majibu ya maswali
yao msingi; wakiburudishwa pamoja na kuhamasishwa kushirikisha kipaji chao cha akili
na ujuzi. Mitandao hii inaendelea kuwa ni sehemu ya vinasaba vya Jamii, kwa kuwawezesha
watu kukutana katika masuala ya msingi. Mitando ya Kijamii inarutubishwa kutokana
na mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu. Baba Mtakatifu
anasema, utamaduni wa mitandao ya Kijamii na mabadiliko katika mtindo wa mawasiliano
ni changamoto kubwa kwa wale wanaotaka kuzungumzia kuhusu ukweli na tunu msingi za
maisha ya binadamu. Jambo hili linaonekana kuwa na ushawishi mkubwa kutokana na umaarufu
wa mtu au mvuto alionao na wala si katika mantiki ya mjadala uliopo kwenye Jukwaa.
Wakati mwingine sauti yenye amani na utulivu inaweza kumezwa na mafuriko ya habari
kiasi kwamba, inashindwa kutoa mvuto unaokusudiwa. Mitandao ya Kijamii inahitaji
kwa namna ya pekee: majitoleo ya watu wanaotambua fika umuhimu wa tunu za majadiliano
zinazosimikwa katika uwezo wa mtu kufikiri pamoja na mpangilio wa mantiki; kwa ajili
ya watu wanaotaka kuunda hotuba na maelezo yanayopania kudumisha mchakato wa mawasiliano.
Kongamano na Majadiliano yanaweza kustawi ikiwa kama watatambua tofauti zao katika
tamaduni pamoja na kuthamini tamaduni za watu wengine ili kutoa fursa ya kuweza kutajirishwa
nazo kwa kutambua kwamba zinafumbata: wema, ukweli na uzuri. Baba Mtakatifu anabainisha
kwamba, mitandao ya Kijamii inakabiliwa na changamoto ya kuifanya kuwa ni shirikishi
kiasi kwamba, itaweza kunufaika na uwepo wa waamini wanaotaka kushirikisha ujumbe
wa Yesu na tunu msingi za utu na heshima ya binadamu zinazotangazwa katika Mafundisho
ya Yesu. Waamini wanatambua kwamba, Habari Njema ya Wokovu inapaswa kufahamika katika
ulimwengu wa mtandao kwani hili pia ni jambo msingi katika mang’amuzi ya wengi. Mazingira
ya mtandao yanagusa uhalisia wa mang’amuzi ya kila siku katika maisha ya mwanadamu,
na kwa namna ya pekee miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Mitandao ya Kijamii ni
matokeo ya mwingiliano wa binadamu yanayoleta mwelekeo mpya katika masuala ya mawasiliano
yanayojenga uhusiano: kwa kuzingatia uelewa huu wa mazingira linakuwa ni jambo msingi
kuweza kuwepo mahali hapo. Kuna haja ya kuwa na uwezo wa kutumia lugha mpya itakayosaidia
kufikisha utajiri wa Injili katika akili na mioyo ya watu wote. Katika mazingira ya
mtandao maandishi kwa kawaida yanasindikizwa na picha pamoja na sauti. Mawasiliano
makini kama ilivyokuwa kwenye mifano iliyokuwa inatolewa na Yesu katika mafundisho
yake yanapaswa kushirikisha kipaji cha ufahamu na mguso kwa wale wanaotaka kutoa mwaliko
wa kukutana na Fumbo la Upendo wa Mungu. Tunatambua kwamba, Ukristo umekuwa na
utajiri mkubwa wa alama na vielelezo: kwa mfano Msalaba, Picha, Sanamu za Bikira Maria,
Pango la Noeli, Madirisha ya Makanisa yaliyopambwa kwa vioo vyenye picha za rangi.
Sehemu kubwa ya amana ya urithi wa mwanadamu imetengenezwa na wasanii pamoja na wanamuziki
waliotamani kuelezea kweli za imani. Baba Mtakatifu anasema, waamini katika mitandao
ya Kijamii wanaonesha ukweli kwa kushirikisha undani wa chemchemi ya furaha na matumaini
yao: imani kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aliyejifunua kwa njia ya
Yesu Kristo. Wanashirikisha ukweli huu kwa njia ya imani na ushuhuda wao kwa jinsi
wanavyowasiliana, chaguzi, vipaumbele na hukumu zao mintarafu Injili, hata kama haijaelezwa
kinaga ubaga. Ushuhuda huu unajionesha kwa mtu kujitoa nafsi yake kwa ajili ya
wengine wanaposhirikisha kwa utulivu na adabu maswali na mashaka yao wanapoendelea
na mchakato wa kutafuta ukweli na maana ya maisha. Ukuaji wa majadiliano katika mitandao
ya Kijamii kuhusiana na imani inaonesha umuhimu na ukuu wa dini katika mihadhara na
maisha ya Kijamii. Baba Mtakatifu anasema kwamba, kwa wale waliopokea zawadi ya
imani kwa moyo mkunjufu, upendo mkuu, ukweli na maana ya maisha; mambo ambayo pia
yanapatikana katika mitandao ya Kijamii wanatambua kwamba yanapatikana kwa Yesu Kristo.
Ni kawaida kwa watu wenye imani kutaka kuishirikisha kwa heshima na taadhima kwa wote
wanaokutana nao katika Jukwaa la Mtandao. Ikumbukwe kwamba, jitihada za Waamini kushirikisha
Injili zitazaa matunda yanayokusudiwa watambue kwamba, hapo kuna nguvu ya Neno la
Mungu inayogusa mioyo ya watu kabla hata ya jitihada zinazofanywa na binadamu. Hata
katika mitandao ya Kijamii kuna sauti kali na yenye mamlaka inapaswa kuoneshwa hasa
pale ambapo sauti zisizoweza kuvumilika zinapotaka kutawala, kwa kuwa makini zaidi
katika maamuzi kwani wakati mwingine Mwenyezi Mungu anazungumza katika sauti nyororo
isiyokuwa na nguvu wala vitisho. Ikumbukwe kwamba, binadamu anatamani kupenda na kupendwa
sanjari na kupata maana ya maisha, hamu ambayo kimsingi imewekwa na Mwenyezi Mungu
mwenyewe katika moyo wa kila mtu ili uweze kuwashwa na mshumaa wa imani. Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake kwa siku ya 47 ya Mawasiliano
Duniani kwa Mwaka 2013 anabainisha kwamba, mitandao ya Kijamii ni njia za Uinjilishaji
na kikolezo cha maendeleo endelevu; ni kichocheo cha umoja na mshikamano miongoni
mwa Jumuiya za Waamini. Mitandao inasaidia kushirikishana rasilimali katika maisha
ya kiroho na kiliturujia; kwa kusali pamoja na wale wanaoshirikishana na kumegeana
imani. Mawasiliano ya kweli na shirikishi yanayohusiana na masuala pamoja na
mashaka ya wale wanaoacha imani, yawasukume waamini kutambua na kuonja umuhimu wa
kuboresha imani kwa njia ya sala na tafakari; kwa kutambua uwepo wa Mungu na kwa njia
ya matendo ya huruma yanayoonesha imani katika matendo. Kuna baadhi ya mitandao
ya Kijamii inayotoa fursa kwa ajili ya sala, tafakari pamoja na kushirikishana Neno
la Mungu. Kuna mitandao mingine inayoweza pia kutumika kwa ajili kufungua malango
kwa masuala mengine ya kiimani. Watu wengi wanaendelea kugundua kwamba, licha ya kukutana
hapo awali kwenye mtandao, lakini bado kuna umuhimu wa kukutana ana kwa ana; kuwa
na mang’amuzi ya Jumuiya na hata wakati mwingine kufanya hija za maisha ya kiroho;
mambo ambayo ni muhimu sana katika hija ya imani. Katika jitihada za kuhakikisha
kwamba, Injili inaingia katika mitandao ya Kijamii, Waamini wanaweza kuwaalika watu
kukusanyika pamoja kwa ajili ya sala au kushiriki katika Liturujia Kanisa au katika
Kikanisa. Umoja na mshikamano wa kiimani ni mambo msingi kama sehemu ya kutolea ushuhuda
wa imani na Injili ya Kristo, iwe ni duniani au katika mitandao ya Kijamii, daima
wako karibu na wengine na wanaalikwa kuwaonjesha upendo wa Mungu watu wanaoishi miisho
ya dunia. Kwa maneno haya, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita anahitimisha
ujumbe wake kwa Siku ya 47 ya Mawasiliano Duniani kwa Mwaka 2013.
Imeandaliwa
na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.