2013-05-11 07:05:56

Papa Fransisko: Kanisa ni Unyenyekevu, Ujasiri, Uwazi na njia ya wote


Wachambuzi wa mahubiri ya Papa , wakitazama mafundisho ya Papa Frasisko, tangu achaguliwe kuwa Papa, ikiwa zimebaki siku chache kutimia miezi miwili kamili wanasema, ujumbe wake katika mahubiri anayoyatoa kila siku asubuhi katika Ibada anazo ziongoza katika Kikanisa cha Mtakatifu Marta kila siku asubuhi, ni juu ya tabia na utambulisho wa Kanisa, ambao ni kielelezo cha unyenyekevu na moyo wa shujaa katika kumsikiliza Roho Mtakatifu.
Hili limebainishwa na Gazeti la L’Osservatore Romano, ambamo mna maeelzo kwamba Papa Fransisko, amefanya rejea nyingi katika kitabu cha Matendo ya Mitume , juu ya maisha ya jamii ya kwanza ya Kikristo ya Yerusalemu, akitazama kwa makini utambulisho wa kanisa na utume tangu mwanzo wa Kanisa.

Maelezo yake yanalitaja kanisa kuwa ni unyenyekevu na ushupavu, wa kuisikiliza Roho Mtakatifu, na ambalo hutoka nje lenyewe kwa ushupavu, kwenda katika kila pembe ya dunia, kwa nia ya kuhubiri kile linacho kiamini, Injili ya Upendo wa Yesu Kristu, aliyesulubiwa kufa na kufufuka katika wafu kwa ajili ya kumkomboa binadamu.
Kwamba Kanisa ni mama, na si yaya. Kanisa hujenga madaraja ya upendo kati ya watu, huwakutanisha na si kuejnga kuta za kutenganisha watu. Milango ya Kanisa ni wazi, likijulikana kama ni jumuiya ya upendo na si kama ni shirika au chama cha kujitegemea au NGO.
Katika kipindi hiki cha chini ya miezi miwili, Papa Francisko ametoa tafakari nyingi kwa waamini, kwa lugha nyepesi lakini yenye kutoa maana ya kina, juu ya maana ya kuishi ndani ya Kanisa, na maana ya kuwa msharika wa Kanisa. Daima anakumbusha kwamba, kwanza zaidi ya yote, kila mbatizwa, anawajibika kuliendeleza Kanisa. Kumtangaza Kristo, akiwa kweli Mkristo hai katika imani, na si kama wakili, bali mhusika kamili, aliyepokea zawadi ya ubatizo, inayotufanya kusonga mbele kwa nguvu za Roho Mtakatifu, katika kumtangaza Yesu Kristo. Hiyo ndiyo maana kuwa Mkristu. Daima ni kutembea katika njia hii ya imani bila kusimama.
Papa Francisko anaasa, pale Kanisa linapopoteza ujasiri huu, wa kuitangaza Injili ya Kristu, kanisa hilo hupoteza umotomoto wa roho wake na hivyo kuwa na ubaridi. Ubaridi huo, huliumiza Kanisa kwa kiasi kikubwa , kwa sababu, hurudisha nyuma asili ya utendaji wake, na hivyo ndani mwake mnazuka matatizo kati ya Waaamini, na kuupoteza mwelekeo jasiri wa imani na sala za kuelekea mbinguni, ujasiri wa kutangaza Injili.
Papa Francisko, hata hivyo anaonya , ujasiri huo, tunauona t, kwa kupata uelewa wa kulipokea Neno la Mungu kwa moyo wa unyenyekevu , na utulivu wa moyo, na kutompinga Roho Mtakatifu. Na hivyo ndani ya Kanisa, tunapata maana ya kuwa kweli jumuiya halisi, inayodumu katika upendo wa Kristo.

Papa Francisko amekuwa akiasa, Sisi, waamini wa kanisa , wanawake kwa wanaume tuliyomo ndani ya Kanisa, ni sehemu ya historia hii ya upendo , kila mmoja wetu ni kiungo katika mnyororo wa upendo . Kama hili hatulielewi , kamwe hatuwezi kuelewa Kanisa ni kitu gani.

Papa pia amekuwa akionya juu ya hatari za kujitenga mbali na kanisa ,hasa wakati wa misukosuko na majaribu ya kujenga Kanisa katika kipimo chetu. Mara kwa mara anarudia kusisitiza kwamba, Njia ya Yesu si itikadi na uzushi unaotafuta faida binafsi , lakini ni njia inayo onyesha mwelekeo wa kweli, hasa pale linapokabiliwa na dhoruba za matatizo na majaribu. Pale linapo shinikizwa na itikadi za malimwengu, au pale roho wa malimwengu anaposhinikizwa ndani mwake na imani isiyo toka kwa Bwana na madhaifu mengine yaliyo lifanya kanisa kupoteza onjo lake la kuwa mshindi dhidi ya mambo ya kilimwengu.
Waamini wanapaswa kukumbuka Kanisa lisilokuwa ujasiri wa ushindi wa Injili, ushindi wa kuupeleka ujumbe wa Injili ya Msalaba,na kashfa ya Msalaba kwa watu wote, haliweza kusonga mbele katika kupambana na malimwengu. Na hivyo huingia katika hatari za kurudi nyuma.








All the contents on this site are copyrighted ©.