Mpendwa mwanatafakari wa Neno la Mungu leo tunasherehekea Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni
Baada ya kazi ya kichungaji na kimisionari hapa duniani Bwana lazima akatoe taarifa
kwa Baba yake.
Kumbe, anapaa
mbinguni kwenda pia kutayarisha makao kwa ajili yetu sote. Anachotaka tufanye kabla
ya kupaa kwake anasema mweni mashahidi wa mateso, kifo na ufufuko wangu na kwamba
kwa njia hiyo mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la
dhambi. Bwana anahaidi zawadi ya Roho Mtakatifu ambayo ilikuwa ahadi ya Baba yake.
Ujumbe huu tunaupata katika somo la injili.
Sherehe ya kupaa mbinguni ni sherehe
ambayo huja siku kumi kabla ya pentekoste, kumbe ni sherehe ya hitimisho la maandalizi
siku 40 kwa Mitume wanapomsubiri Roho Mtakatifu, wanaposubiri kuanza kazi yao ya kitume.
Kupaa ni kuingia katika utukufu wa Mungu na kuachana na kifungo cha kifo. Ni kutenganisha
dunia yetu na Mungu na hasa ni kuwa karibu na Mungu.
Kristo anapopaa mbinguni
anaingia katika utukufu wa Mungu, ni utukufu ambao hatuwezi kuugusa bali kwa njia
ya imani tunaweza kuufikia. Hata hivyo Bwana kabla ya kupaa katika kipindi cha siku
40 anatoa wosia mbalimbali: Anawaambia Mitume wasitoke Yerusalemu hadi ahadi ya Baba
yake itimie yaani ya kuwapelekea Roho Mtakatifu atakayewasidia katika utume wao, yaani
watatenda na kubatiza katika Roho Mtakatifu. Anawaambia watapokea Roho wa Mungu na
watakuwa mashahidi katika Uyahudi na Samaria yote. (Mdo 1:8).
Mpendwa ujumbe
huu si kwa ajili ya mitume tu bali kwa ajili ya Kanisa zima, ndiyo kusema tuaalikwa
kuitikia wosia wa Mungu daima ambao tunaupata kwa njia ya Neno lake na hasa kuwa mashahidi
wa upendo kwa mataifa kama tulivyosikia dominika iliyopita.
Mtume Paulo anakazia
imani katika Bwana Mfufuka anapowaandikia Waefeso anawakumbusha kuwa Kristu ni mfufuka
na ni kichwa cha Kanisa ameketi kuume kwa Mungu na atawala falme zote za dunia. Anasema
maisha yao hayafungwi na ulimwengu bali wanaalikwa kuishi katika tumaini la kumsubiri
Kristo ajaye. Mpendwa nasi tunaalikwa pia kukumbuka kuwa sisi si watu wa ulimwengu
huu, bali tukishafufuliwa, tunatazama yaliyo ya juu, tunaishi pamoja na Kristo.
Mpendwa,
Bwana anapopaa kuna matukio ambata yanayotokea. Kwanza kuna watu wawili wenye nguo
nyeupe, hawa ni wawakilishi wa utakatifu wa Bwana, ni alama ya uwepo wa Mungu pamoja
na Kristo, kumbuka pale kaburini yule aliyekuwa amekalia jiwe! Maneno waliyoyasema
hawa watu wawili ni ujumbe toka kwa Mungu, yafaa na ni lazima kuyatimiza. Linatokea
wingu, hili latukumbusha safari ya Waisraeli kule jangwani wakitoka Misri, waliongozwa
na Mungu kwa njia ya wingu, na hivi wingu ni ishara ya uwepo wa Mungu. Kut.13:22.
Mitume
na wengine yaani watu wa Galilaya wanatazama juu na kisha ujumbe unatoka ukiwaambia
vivyohivyo alivyokwenda ndivyo atakavyorudi. Kutazama juu kadiri ya wanamaandiko ni
kumwelekea Mungu lakini pia watukumbusha kuhangaikia upendo hapa duniani ili kutazama
kwetu juu kuwe na mzizi wa upendo uliojaa wajibu wa huduma kwa walio na mahitaji ya
kiroho na kimwili.
Mpendwa shamrashamra za kupaa Bwana zinaambatana na wajibu
wa kuhubiri injili kwa kila kiumbe kwa mataifa na kwa nguvu mpya ya Bwana. Na katika
kuhubiri, mwinjili anatuhakikishia ukuu wa kusadiki kwamba hatutweza kudhuliwa na
kitu chochote cha kufisha. Basi ni kwa jinsi hiyo nakualika unaposhangilia kupaa Bwana
uweke nia ya pekee kwa ajili ya kazi ya kimisionari kwa njia ya sala na majitoleo
mbalimbali katika familia na kanisa kwa ujumla.
Mpendwa nikutakie furaha na
mapendo ukisubiri ujio wa Roho Mtakatifu Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C. PP.S.