2013-05-10 08:36:10

Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu katika huduma za kijamii


Sr. Maria Eugenia Thomas, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu ni kati ya Mama Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa uliomalizika hivi karibuni kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko hapa mjini Vatican. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu aligusia kuhusu nadhiri ya utii kwa kusema kwamba, ni njia mahususi ya kusikiliza na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha ya mtawa, akiongozwa na Roho Mtakatifu anayetenda kazi ndani mwake na kwa njia ya wakuu na viongozi wengine wa Kanisa.

Ufukara ni nadhiri inayomwilisha mshikamano wa upendo kwa njia ya matendo ya huruma ili kutambua maana halisi ya maisha. Ufukara ni nadhiri ambayo mtu anajifunza kuimwilisha kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; wagonjwa, wazee na watoto wanaohitaji huduma.

Baba Mtakatifu Francisko alisema kwamba, nadhiri ya usafi wa moyo ni zawadi ya uhuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwonjesha mtawa: upendo, huruma na upole wa Kristo, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu. Umama wa watawa ni kielelezo cha Umama wa Bikira Maria na Kanisa.

Katika mahojiano na Radio Vatican, Sr. Maria Eugenia Thomas anasema, Shirika la Masista wa Kazi za Roho Mtakatifu lilianzishwa na Mheshimiwa Padre Benhard Bendel nchini Ujerumani kunako mwaka 1950 ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha iliyojitokeza mara tu baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia. Watu wengi walijikuta wakikabaliana na hali ngumu ya maisha, kiasi cha kukata tamaa. Padre Bendel akasoma alama za nyakati na kujipanga ili kuwasaidia watu kwa njia ya mikakati ya shughuli za kichungaji pamoja na kuyashughulikia masuala ya kijamii kwa wakati huo.

Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu kunako mwaka 1962 likajipanua nchini Marekani. Mwaka 1964 likafikisha matawi yake nchini Tanzania na kutua nanga Jimbo Katoliki la Moshi. Kunako mwaka 1969 wakafungua Jumuiya nchini India na Ufilippini. Masista waliokuwepo Tanzania wakafungua nao Jumuiya nyingine nchini Kenya na Malawi. Hadi leo hii kuna jumla ya Masista 550, kati yao kuna Masista 220 kutoka Tanzania.

Sr. Maria Eugenia Thomas, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu anabainisha kwamba, wao kama sehemu ya utume wao wanajikita zaidi katika utoaji wa huduma ya afya kwa Mama na Mtoto, elimu, huduma za kijamii pamoja na shughuli za kichungaji Parokiani.







All the contents on this site are copyrighted ©.