Billioni 1.36 za pato la DRC zimepotea katika mazingira ya kutatanisha!
DRC katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2012 imepoteza mapato kiasi cha
dolla za kimarekani zipatazo billioni 1.36 kutokana na zoezi la kupunguza mauzo kwa
baadhi ya Makampuni ya uchimbaji wa madini nchini humo, kadiri ya taarifa iliyotolewa
na Jopo linaloongozwa na Kofi Annan, aliyekuwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika
Jukwaa la Uchumi wa Afrika. Upotevu huu wa fedha ni sawa na bajeti iliyotolewa na
DRC kwa ajili ya Wizara ya Afya na Elimu kwa Mwaka 2012.
Taarifa hii inaonesha
jinsi ambavyo rasilimali na utajiri wa wa Bara la Afrika unavyokwapuliwa na wajanja
wasiozingatia utawala wa sheria, mafao ya wengi wala uzalendo kwa nchi yao. Kutokana
na hali hii kuna haja ya kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini mahali ambapo fedha
hizi zimetokomea kwa kuyahusisha makampuni yanayojishughulisha na uchimbaji wa nishati
na madini nchini DRC. Jopo hili linasema kwamba, hizi ni dalili za rushwa, ufisadi
na ukosefu wa misingi ya ukweli na uwazi.