2013-05-10 07:33:30

Baadhi ya mambo yanayopelekea kuwepo kwa wimbi kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi!


Tatizo la watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi Barani Afrika linaendelea kuongezeka maradufu kutokana na sababu mbali mbali. RealAudioMP3

Wachunguzi wa masuala ya kijamii wanabainisha kwamba, hali ngumu ya uchumi, magonjwa ya muda mrefu, kuyumba kwa tunu bora za maisha ya kifamilia na kijamii, ndoa tenge, ukatili wa wazazi pamoja na utukutu wa watoto ni kati ya mambo ambayo yamepelekea watoto wengi Barani Afrika wakijikuta kila siku wakirandaranda kwenye miji mikuu kutafuta riziki yao. Hili ni kundi ambalo linatishia amani na usalama wa wananchi kutokana na kukosekana kwa misingi bora ya maadili na utu wema.

Shirika la Habari za Kimissionari la FIDES linaonesha kwamba, mjini Dakar, Senegal kuna zaidi ya watoto 20,000 wanaoishi katika mazingira magumu, ambao wanalazimika kuranda randa mitaani kila siku ili kutafuta mahitaji yao pengine na ya familia zao. Taarifa ya Shirika lisilo la Kiserikali lijulikanalo kama “Employment Non Discrimination Act, (ENDA), linasema kuna zaidi ya watoto millioni 250 wanaoishi katika mazingira magumu duniani. Hali hii inatisha hasa Barani Asia na Afrika.

ENDA inabainisha kwamba, hii inatokana na kuongezeka kwa watoto yatima ambao wanaachwa na wazazi na ndugu zao kutokana na ugonjwa wa Ukimwi na magonjwa mengine ya kuambukiza. Watoto wanaoishi katika mazingira magumu ni matokeo pia ya migogoro, kinzani na vita inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaonesha madhara makubwa katika maisha ya kifamilia, kiasi kwamba watoto wengi wanaamua kukimbia kutoka katika familia zao wakiwa na tumaini la kupata nafuu ya maisha mijini, lakini wanapofika huko wanajikuta wakiteseka zaidi kuliko walivyokuwa wakiishi kwenye familia zao.

Mashirika yanayojihusisha na haki msingi za watoto yanaonesha kwamba, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wakati mwingine wanakumbana na madhulumu, nyanyaso na hata kubaguliwa, kwani kwa watu wengi watoto hawa wanahesabiwa kuwa ni vibaka, wezi na changudoa.

Umefika wakati kwa Jamii kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kuwajengea uwezo watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa njia ya elimu itakayowawezesha kuboresha hali ya maisha yao pamoja na kupewa ulinzi na usalama dhidi ya watu wenye nia mbaya wanaoweza kuwatumia watoto hawa kwa ajili ya mafao yao binafasi, kama ambavyo inejionesha hadi sasa.








All the contents on this site are copyrighted ©.