Wananchi wa Baga, Kaskazini mwa Nigeria bado wana hofu ya kuzuka tena kwa mapambano!
Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Nigeria kinasema kwamba, tangu yalipotokea mashambulizi
kwenye Kitongoji cha Baga, Kaskazini mwa Nigeria hivi karibuni, watu wengi bado wanahofia
kurudi kwenye makazi yao kutokana na wasi wasi wa kuzuka kwa mapigano kati ya Kikosi
cha Kimataifa cha kulinda amani (MNJTF) na Kikundi cha Boko Haram ambacho kimekuwa
ni tishio la maisha ya watu na mali zao nchini Nigeria. Katika tukio hilo nyumba 2,275
zilichomwa moto na nyingine 125 zikaharibiwa kiasi kwamba, hazifai tena kwa matumizi
ya binadamu.
Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Nigeria kwa sasa kimeandaa
makazi ya muda kwa watu wasiokuwa na makazi wapatao 600. Hali ya maisha bado ni ngumu
kwani wakazi wa eneo hili wanategemea sekta ya uvuvi na kilimo kwa ajili ya kujipatia
mahitaji yao msingi. Wananchi wa Baga watahitaji msaada wa pembejeo za kilimo ili
kukabiliana na hali ngumu ya maisha waliyo nayo kwa sasa.