Utamaduni wa kifo unaoendelea kukua na kukomaa miongoni mwa wananchi wa Canada umepelekea
vifo vya watoto wengi wa kike nchini humo; watoto ambao wananyimwa haki ya kuonja
upendo kutoka wazazi na Jamii inayowazunguka hata kabla ya kuzaliwa.
Kanisa kamwe
haliwezi kuvumilia kuona watu wanatema zawadi ya maisha kutokana na ubinafsi na kwamba,
waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Canada wanapaswa kusimama kidete kulinda
na kutetea Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa Mama yake!
Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Chama cha Kitume cha Kutetea Maisha na
Familia kutoka Kanisa Katoliki nchini Canada, kama sehemu ya Maandalizi ya Maandamano
kwa ajili ya kutetea maisha, yatakayofanyika kitaifa hapo tarehe 9 Mei 2013 kwa kuweka
kipaumbele cha kwanza kutetea uhai wa watoto wa kike ambao wanaendelea kutolewa mimba
kutokana na ukweli kwamba, wananchi wengi wa Canada wanapendelea kuwa na watoto wa
kiume kuliko kuwa na watoto wa kike!
Lakini ikumbukwe kwamba, maisha ni kati
ya tunu msingi zinazopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika Familia na Jamii kwa
ujumla, kwa bahati mbaya, maisha yamekuwa yakipigwa danadana kama mpira na watu wanaokumbatia
utamaduni wa kifo kwa masilahi yao binafsi kwa madai kwamba, wanatetea haki ya utoaji
mimba inayosigana kimsingi na haki ya maisha ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi
Mungu.
Utoaji mimba ni mauaji. Miaka saba imepita tangu wananchi wa Canada
walipojulishwa kwamba, nchini mwao kulikuwa na dhana ya kuchagua ni mtoto wa jinsia
gani anaweza kuzaliwa kutokana na utashi wa wazazi au mzazi husika, jambo ambalo lilipelekea
utoaji mkubwa wa mimba za watoto wa kike. Haya ni maendeleo ya sayansi katika masuala
ya uzazi, lakini yamekuwa na athari kubwa katika kuenzi Injili ya Maisha kwa madai
kwamba, lengo ni kuendeleza huduma ya afya ya uzazi kwa wanawake wajawazito; huduma
ambayo wachunguzi wa masuala ya kimaadili na utu wema wanasema inakumbatia utamaduni
wa kifo.
Nchini Canada kumeibuka mtindo wa watu kutamani watoto wa kiume kama
warithi dhidi ya watoto wa kike. Chama cha Kitume cha Kutetea Maisha na Familia Kanisa
Katoliki nchini Canada, kinawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama
kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai, utu na heshima ya binadamu bila ubaguzi
kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Umefika wakati wa kuachana
na utamaduni wa kifo unaofanywa na baadhi ya watu katika Jamii kwa masilahi yao binafsi
na kwamba, kuna hatari kubwa kwa watoto wa kike kuendelea kutolewa mimba.
Wananchi
wajenge utamaduni wa kuenzi usawa katika utu wa binadamu tangu pale mtoto akiwa bado
tumboni mwa mama yake. Waamini na wananchi wa Canada kwa ujumla, wanaalikwa kushikamana
ili kuonesha kwamba, wanapinga vitendo vya utoaji mimba kwa kushiriki na kuunga mkono
kwa vitendo maandamano makubwa yatakayofanyika hapo tarehe 9 Mei 2013 kuzunguka Bunge
la Canada.