2013-05-08 15:53:37

Mkristu hapaswi kuwa mtu wa kulalamikia mateso na dhiki bali ..


Papa Francesco amesema, Mkristo mzuri si mtu wa malalamiko lakini hukabiliana na machungu kwa furaha katika ukimya wa amani.

Hata katika kuzingirwa na mateso na dhiki, Mkristo, kamwe hapaswi kuwa mtu wa kulalamika tu , bali anapaswa kuyaishi mazingira hayo, kama wakati wa kumkomaza katika kumshuhudia Kristu kwa furaha.

Papa Francis, aliasa wakati wa Ibada ya Misa, katika kanisa dogo la Mtakatifu Marta, mapema siku ya Jumanne .Papa aliiongoza Ibada hiyo kwa kusaidiana na Kardinali Angelo Comastri, na Kardinali Jorge Mejia, washiriki wengine wakiwa ni kundi la wafanyakazi Kiwanda cha Mtakatifu Petro, cha Vatican.
Papa katika homilia yake, alisistiza kwamba, hata katika dhiki, Wakristo wanapaswa kupokea dhiki hizo kwa matumaini na furaha na si kuhuzunika. Papa alieleza kwa kukazia juu ya furaha ya Paulo na Sila, walipokabiliwa na mateso hadi kutupwa gerezani kwa tuhuma za kushuhudia Injili. Walipokea mateso hayo kwa furaha, kwa sababu walijua kile wanachokitetea wakiwa wamejawa na furaha na matumaini ya kumfuata Yesu katika njia ya mateso yake. Njia iliyofuatwa na Bwana kwa uvumilivu.

Papa aliendelea kufafanua kwamba, uvumilivu wa kuifuata ile njia ya Yesu pia hutufundisha sisi Wakristu, manufaa ya kina cha uvumilivu wa imani kwa kristu, badala ya kuwa na hofu na huzuni kw amateso tunayoyapata kutokana na imani yetu kwa Kristu. Hii ina maana ya kubeba, kubeba juu ya mabega mwetu , uzito wa matatizo, uzito wa utata, uzito wa mateso, kama tabia ya Mkristo inayomwingiza katika tabia ya uvumilivu .

Na kama ilivyoelezwa katika Biblia, katika neno la Kigiriki,” hypomone”, kuvumilia katika utendaji wa kazi za maisha ya kila siku, ambamo mna kukumbana na utata, majonzi, na mengine mengi. Paulo na Sila walibeba dhiki zao kwa kuvumilia udhalilishwaji: kama Yesu alivyovumilia wakati wa mateso yake. Huu ni mchakato, mchakato unaojenga ukomavu kwa Mkristo, kupitia njia ya uvumilivu. Ni mchakato wa mapito ya muda unaojitokeza siku hadi siku, ukimkomaza Mkristu katika njia yake ya maisha ya ukomavu kwa Kristo, kama ilivyo njia ya kuipata divai nzuri. "

Papa aliwakumbuka mashahidi wengi wa imani walio yapokea mateso yao kwa furaha, kama vile mashahidi wa Nagasaki walivyosaidiana mmoja kwa mwingine, kukabiliana na kifo. Na mashahidi, wengine wengi ambao, walisubiri kwa furaha kifo chao kama vile wanakwenda kwenye sherehe ya arusi. Papa ameomba wakristu kuifanya tabia hii ya uvumilivu, iwe tabia sugu ya Mkristu wa kweli .

Tabia inayonekana katika maisha ya kawaida ya Kikristo, tabia ya kupata ashiki ya kufurahia mateso kwa ajili ya imani, kuwa mwelekeo wa kutembea katika njia ya maisha na Yesu.

Papa pia ameasa kwamba , mara nyingi, dhiki na mateso huja na vishawishi na majaribu mengi. Na alitoa mfano kwamba, wakati wa maombolezo, Mkristu pamoja na uchungu wa mateso na dhiki hapaswi kuwa mtu wa kulalama kila wakati. Badala yake anatakiwa kuwa katika ukimya, kimya cha uvumilivu. Ukimya wa Yesu: Yesu katika Mateso yake hajazungumza zaidi ya mara mbili au tatu ... Lakini alikubali kutembea na mateso na dhiki, katika hali ya kimya cha huzuni, ukimya wa kubeba Msalaba, lakini si ukimya wa kudhoofisha furaha ya ndani ya moyo.
Moyo wake ulikuwa na amani. Paulo na Sila walikuwa wakiomba kwa amani. Walikuwa na uchungu, lakini Bwana aliwafuta machozi yao na kuwasafisha majeraha yao gerezani – yote waliyavumilia kwa amani. Njia hii ya mateso inatusaidia kuzama katika kuiimarisha amani ya Kikristo, na katika Yesu tunafanywa kuwa na nguvu za kukabiliana na yote.

Hivyo basi Mkristo unaalikwa kama Yesu alivyofanya, "bila ya malalamiko, kuvumilia kwa amani." Aliendelea, Papa Francesco, kwenda kwa uvumilivu,imani yetu hufanywa upya kama kijana. Ujana a imani ya ndani.

Papa alieleza na kutolea mfano wa watu wazee au wazee katika nyumba ya mapumziko, ambao wamevumilia sana katika maisha, na kwa sasa tunawaona kama vile, wamerudi kuwa kama watoto wadogo, wamefanywa kuwa wapya, na tunawatazama kwa macho ya ujana, ujana wa kiroho. Kwa namna hiyo , Bwana anatualika sote katika ujana wa Pasaka hii, kufanywa upya katika njia ya upendo na subira, kuvumilia mateso na pia katika kusaidiana mmoja kwa mwingine.
Kwa ajili hii, Papa ametoa mwaliko kwamba, tunapaswa kutenda kwa ukarimu na upendo , tukisaidiana mmoja kwa mwingine , na kwa namna hiyo , tusonge mbele katika njia ya kutembea na Yesu . Tumwombe Bwana, neema za kusaidia Wakrtistu kuwa na amani zaidi ndani ya mioyo yao , msaada wa furaha na ujana zaidi wa kiroho , ujana mpya wa Pasaka hii na Roho mpya. Na iwe hivyo.








All the contents on this site are copyrighted ©.