Kardinali Pengo: simameni kidete kusema na kutetea ukweli ili kujenga amani!
Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Baba Mtakatifu Yohane
wa Ishirini na tatu alipochapisha Waraka "Pacem in Terris" "Amani Duniani" anakumbusha
kwamba, amani kimsingi inasimikwa katika mihimili mikuu minne: Yaani: Ukweli, haki,
uhuru na upendo unaojionesha katika mshikamano wa dhati baina ya watu ndani ya Jamii.
Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, akirejea
kuhusu tukio la kigaidi lililotokea Jimbo kuu la Arusha, Jumapili tarehe 5 Mei 2013
na kusababisha maafa makubwa anasema, amani ya kweli nchini Tanzania itajengwa katika
msingi wa ukweli bila kuupotosha wala kuupindisha. Watu wajifunze kusimama kidete
kusema na kutetea ukweli!
Kardinali Pengo anakazia kwamba, amani ya Tanzania
ni jambo la msingi linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Kujaribu kuficha au kupotosha
ukweli ni kutaka kumfungulia njia Ibilisi ili aweze kuleta vurugu na kinzani miongoni
mwa Watanzania.